Naibu Sheha afungwa miaka 10 kwa utoroshaji, ubakaji Pemba

 

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

NAIBU Sheha wa shehia ya Mgogoni wilaya ya Chakechake Mwadini Ali Mwadini, maehukumiwa kwenda chuo cha mafunzo, kwa muda wa miaka 10, na kulipi fidia ya shilingi milioni 2 sambamba na faini ya shilingi milioni 1, baada ya kupatikana hatia ya kutorosha na kumbaka mtoto wa miaka 13 wanaeishi kijiji kimoja.

Mshitakiwa huyo aliekuwa rumande tokea Septemba 9 mwaka huu, akikabiliwa na makosa hayo, juzi Novemba 11, mwaka huu alipanda mahakama ya Mkoa Chakechake ‘A’ chini ya Hakimu Abdullarazak Abdullakari Ali, na Mwendesha Mashitaka Mohamed Ali Juma kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka Pemba, kwa lengo la kusomewa hukumu yake.

Awali Mwendesha mashitaka huyo alisema kuwa, kesi hiyo ipo mahakamani hapo kwa ajili ya kusomea hukumu, baada ya wiki mbili zilizopita, upande wa mashitaka kufunga ushahidi na mshitakiwa kukamilisha utetezi wake mahakamani hapo.

Baada ya kupanda kizimbani hapo, mshitakiwa huyo akisubiri kusomewa hukumu yake, ndipo hakimu wa Mahakama hiyo ya Mkoa ‘A’ Chakechake, alipomueleza kuwa, atatumikia chuo cha mafunzo kwa muda wa miaka saba (7), kwa kosa la ubakaji na atatumikia miaka mitatu (3), kwa kosa la pili la utoroshaji wa mtoto.

Hakimu huyo alimueleza mshitakiwa huyo kuwa, kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani na mashahidi mbali mbali ikiwa ni pamoja na Polisi mpelelezi, mtoto mwenyewe, mama mzazi, daktari umeitosheleza mahakama kumtia hatiani.

“Mshitakiwa kutokana na ushahidi uliotolewa, mahakama hii ya Mkoa Chakechake ‘A’ umeridhishwa na bila ya kuacha shaka yoyote, ndio maana unatakiwa kutumikia chuo cha mafunzo kwa miaka 10 na kulipa fidia ya shilingi milioni 2 na faini ya shilingi milioni 1,’’alisema Hakimu huyo.

Awali mashitakiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo, Septemba 9 mwaka huu, akikabiliwa na kosa la utoroshaji na ubakaji wa mtoto wa miaka 13.

Mwendesha Mashitaka kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa mashitaka kisiwani Pemba Mohamed Ali Juma, alisema kuwa, alitenda kosa hilo August 19 mwaka huu.

Alisema kuwa, kosa hilo lilifanyika majira ya saa 2:35 usiku wakati mtoto huyo akiwa katika eneo akiangalia tv na kisha baada ya kufanikiwa kurubuni, alimpelekea kichakani (migombani) na kumbaka.

“Wewe Mwadini Ali Mwadini unalimtorosha mtoto aliechini ya uangalizi wa wazazi wake, na kwenda nae kichakani na kisha huko huko ulimbaka, ukijuwa kuwa ni kosa,’’alisema Mwendesha Mashitaka.

Mara baada ya kusomewa shitaka lake hilo dhidi yake, mshitakiwa kwa wakati huo alikana, na kisha kujikuta akijumuisha na watuhumiwa wengine kwenda rumande kwa muda wa wiki mbili, kabla ya juzi Novemba 11 kutiwa hatiani.

Kumchukua mtoto aliechini uangalizi wa wazazi wake ni kosa kinyume na kifungu cha 113 (1) (a) cha sheria ya Adhabu no 6 ya mwaka 2018, sambamba na kubaka, kuwa ni kosa kwenye kifungu cha 108 (1) (2) (i) na kifungu cha 109 (1) cha sheri hiyo hiyo ya Zanzibar.

Mwisho