Naibu Spika: Tamasha la michezo kuchapuza idadi ya watalii Pemba

 

IMEANDIKWA NA MWANDISHI MAALUM-PEMBA

NAIBU Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe: Mgeni Hassan Juma, amesema kumalizika kwa tamasha la michezo ya Utalii kisiwani Pemba, ni chachu ya ongezeko la idadi ya watalii wanaotembelea kisiwani humo, kutoka 29, 403 kwa mwaka 2018 kuongezeka mara mbili zaidi.

Alisema kabla ya mwaka 2014, kasi ya watalii wanaotembelea kisiwani humo ilikuwa ndogo, lakini kuanzia mwaka huo iliongezeka na kufikia 26,465 na miaka minne baade iliongeza tena na kufikia 29,403 kutokana na mikakati ya serikali.

Naibu Spika alieleza hayo August 3, mwaka huu fukwe ya Vuma wimbi wilaya ya Micheweni Pemba, alipokuwa akizungumza na wananchi, wanamichezo na wageni wengine mbali mbali  kwenye ufungaji wa tamasha la tatu la michezo ya Utalii Kisiwani humo.

Alisema Serikali imekuwa ikibuni mbinu na mikakati imara ya kuhakikisha isiwa cha Pemba na Zanzibar kwa ujumla kinakua kiutalii, kwa lengo la kuongeza pato la mwanachi mmoja moja na Taifa kwa ujumla.

“Bonanza hili la michezo ya Utalii, ni faida kubwa katika kukitangaaza Kisiwa cha Pemba, na naamini wageni kwa mwaka ujao inaweza kuongezeka mara dufu,’’alieleza.

Katika hatua nyingine, Naibu huyo Spika wa Baraza la wawakilishi Zanzibar, alisema bado sekta ya utalii itaendelea kuwa tegemeo katika kukuza uchumi wa Zanzibar, kwa maana imeshatoa ajira za moja kwa moja 30,000 na zisizo moja kwa moja 70,000.

Nae, Naibu waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar Mhe: Chumu Kombo Khamis, alisema mipango na mikakati ya Serikali kwa kushirikiana na wadau wake, imechangia kuongezeka kwa watalii Zanzibar na kufikia 52,809 kwa mwaka 2018.

Alieleza kuwa, idadai hiyo ni tofauti na ile iliorikodiwa mwaka 2012, ambapo Zanzibar kwa mwaka huo ilikepokea watalii 12,440.

“Serikali bado inaendelea kuhakikisha Kisiwa cha Pemba nacho kinakuwa kiutalii na hasa kutokana na fursa zilizopo, kina ongeza idadi ya watalii, maana mwaka 2018 kilipokea watalii 29,000 pekee kati ya watalii 52,809 waliotembea Zanzibar,’’alifafanua.

Bi chumu, alisema anaelewa kuwa katika kukuza pato la wananchi na kuondoa umaskini, sekta ya utalii inalojukumu hilo, kama ilivyobainishwa kwenye MKUZA na dira ya Zanzibar ya mwaka 2020.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara hiyo Khadija Bakari Juma, alisema mbali ya kubadilisha sera na sheria na kisha kutunga sheria mpya ya Utalii ya mwaka 2012, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, imefanya mambo kadhaa katika kuimarisha sekta ya hiyo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara na sekta ya umeme.

“Serikali pia katika kuimarisha sekta ya Utalii, imekuwa ikitenga fedha nyingi katika kuimarisha maeneo ya kihistoria kama vile kwa Bihole Bungu, Dunga kwa Unguja na Mkamandume na hapo baadae Chwaka,’’alifafanua.

Aidha Mwenyekiti wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Sabah Saleh, alisema kilichofanyika Kisiwani Pemba na maeneo mengine na  kusimamia na kuendeleza utalii, ni wajibu wa Kamisheni kisheria.

Alisema tamasha la mwaka huu, limekuwa la aina yake kwa kule kushirikisha mbizo ndefu za baiskeli ‘triathlon’, mbio za Nyika  ambazo ni kwa mara ya kwanza kufanyika, samba mba na kuibua kamati za utalii za Wilaya.

“Napenda kuchukua fursa hii kuziomba kamati hizo, mujipange vyema ili kufanya shughuli mbali mbali za Utalii katika wilaya zenu, kutokana na yalioibuliwa kwenye bonanza hili,’’alieleza.

Hata hivyo Katibu Mkuu huyo, alisema suala la kuimarisha uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Amani Karume kwa kutengewa shilingi bilioni 60, kwenye bajeti ya mwaka 2019/2020, utaziwezesha ndege kubwa kutawa uwanjani hapo ambapo Watalii wanaweza kuongezeka.

Nae Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Dk Abdalla Juma Mohamed, aliwapongeza wote waliochangia katika kufanikisha bonanza hilo la michezo ya Utalii Kisiwani Pemba.

Alisema kwenye Tamasha hilo la tatu, hawezi kuisahau taasisi ya kiraia ya Rafiki Network, kwa kuandaa tamasha hilo kwa mara ya tatu mfululizo Kisiwani humo.

Hata hivyo Katibu huyo Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, alieleza kufuatia kufanyika Kisiwani Pemba kwa tamasha hilo, ni dhahiri wananchi wamepata muamko zaidi wa kushiriki katika shughuli tofauti za kiutalii kwenye maeneo yao.

Bonanza la michezo ya Utalii Kisiwani Pemba ambalo ni la tatu, kwa msimu huu lilichanganya mambo kadhaa ikiwemo mbizo za nyika, mbizo ndefu za kilomita 57 kutoka Mkoani hadi Msitu wa Ngezi na kisha washiriki kwenda mbio kilomita 11 hadi fukwe ya Vuma wimbi.

Uzinduzi wa tamasha hilo wenye lengo la kuongeza idadi ya wageni wa Utalii Kisiwani Pemba, ulianza Julai, 28 kwa michezo ya mbio za nyika, kuogelea, kuendesha baiskeli na kukimbia.

Sekta ya Utalii Zanzibar, imekuwa ikichangia pato la Taifa kwa zaidi ya asilimia 27, na asilimia 80 ya fedha kigeni, ambapo tayari imeshatoa ajira za moja kwa moja 30,000 na zisizo za moja kwa moja 70,000 samba mba na kuchangia kwenye sekta ya kilimo, ujenzi, viwanda na biashara.

Kauli mbiu ya mwaka huu kwenye Tamasha hili la Utalii kwa mwaka 2019 ambalo awali Julai 28 lilifunguliwa na Rais mstaafu wa awamu ya pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe: Ali Hassan Mwinyi ni ‘Utalii kwa wote: huduma bora, faida kwa wote’.

                               MWISHO .