Ni kweli Corona Tanzania imepungua?

 

Rais wa Tanzania John Magufuli amesema wagonjwa wa virusi vya corona katika hospitali mbalimbali nchini humo wamepungua sana, ingawa serikali haijatoa takwimu rasmi za viwango vya maambukizi kwa wiki tatu.

Kiongozi huyo mara kwa mara amesisitiza kwamba watu hawafai kuwa na hofu kuhusu ugonjwa huo. Hatua zake zimeyatia wasiwasi mataifa jirani na mashirika ya kimataifa.

Tanzania imeruhusu safari za ndege za kubeba abiria za kimataifa kurejea na wageni watakaokuwa wakiwasili hawatawekwa kwenye karantini ya lazima ambayo awali ilikuwa siku 14.

Dkt Magufuli ametangaza pia tarehe ya kufunguliwa kwa vyuo na pia kurejelewa kwa michezo nchini humo.

Je, tunafahamu nini kuhusu kuenea kwa virusi vya corona nchini Tanzania?

Kuna takwimu?

Serikali ilisitisha utangazaji wa takwimu za ugonjwa huo mara kwa mara mwezi Aprili baada ya rais kulalamika kwamba desturi ya kutangaza idadi ya wagonjwa ilikuwa inaongeza hofu. Alisema ilifaa pia maafisa kuangazia waliokuwa wanapona ugonjwa huo.

Kituo cha Kudhibiti Magonjwa cha Umoja wa Afrika wiki iliyopita kilitoa wito kwa Tanzania kutoa takwimu na kwa wakati.

Alhamisi wiki hii, kiongozi wa wa Afrika CDC Dkt John Nkengasong alisema Tanzania bado haijawasilisha taarifa kwa kituo hicho ingawa mawasiliano yanaendelea.

Takwimu rasmi za mwisho za Tanzania zilitangazwa 29 Aprili na waziri mkuu ambapo wagonjwa walikuwa 480, na waliokuwa wamefariki kutokana na ugonjwa huo walikuwa 21. Zanzibar baadaye ilitangaza ongezeko la wagonjwa mara moja, mnamo 7 Mei walipotangaza wagonjwa 29 wapya. Hiyo ilifikisha idadi ya wagonjwa Tanzania hadi 509.

Rais Magufuli - hapa akionekana Desemba 2019 - amekosolewa kwa kutotoa takwimu kuhusu maambukiziHaki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Image captionRais Magufuli – hapa akionekana Desemba 2019 – amekosolewa kwa kutotoa takwimu kuhusu maambukizi

Rais Magufuli Jumapili iliyopita alitoa takwimu kiasi kuhusu wagonjwa wa Covid-19 waliokuwa wamelazwa katika hospitali na vituo mbalimbali nchini humo. Alisema idadi ya wagonjwa katika hospitali mbili kubwa jijini Dar es Salaam ilikuwa imeshuka kutoka 228 hadi 18, na kutoa pia takwimu za hospitali nyingine nchini humo. Hata hivyo, hakusema idadi hiyo imeshuka kutoka lini hadi lini.

Ni vigumu kuthibitisha takwimu hizo, na pia ni vigumu kupata takwimu za kiwango cha maambukizi na idadi ya vifo kwa sasa nchini humo.

“Tanzania kwa muda mrefu imekuwa na sheria kali zinazominya uhuru wa kujieleza na uhuru wa wanahabari,” anasema Roland Ebole, ambaye ni mtafiti wa kanda katika shirika la Amnesty International.

“Sasa, tunashuhudia sheria hizo zikitumiwa katika njia kubwa zaidi kuwalenga wale wanaozungumza, hasa kuhusu Covid-19,” anasema Bw Ebole.

Mapema mwezi huu, ubalozi wa Marekani nchini Tanzania ulitoa tahadhari kwamba hospitali nyingi katika jiji la Dar es Salaam zilikuwa “zimezidiwa” wiki za hivi karibuni.

“Hatari ya kuambukizwa COVID-19 Dar es Salaam iko juu mno. Licha ya taarifa rasmi kutotolewa sana, ushahidi wote unaonyesha kwamba kumekuwa na ongezeko kubwa la ugonjwa huu Dar na maeneo mengine Tanzania,” tahadhari hiyo ilisema.

  • Majirani wa Tanzania kuwa na wasiwasi

Kusambaa kwa maambukizi ya virusi hiyo katika maeneo yanayopakana na Tanzania kumekuwa kukiwatia kiwewe majirani wa taifa hilo.

Kuna vituo vya mpakani ambavyo hutumiwa kusafirisha bidhaa, mizigo na watu. Kuna wasiwasi kwamba madereva wa masafa marefu na wasafiri wengine wamekuwa wakieneza virusi hivyo.

Baadhi ya mataifa yamekuwa yakiwapima watu wanaotokea Tanzania wakiingia nchi hizo, mfano Kenya, Zambia na Uganda. Baadhi ya nchi zinawazuia watu kuingia iwapo watagundulika kuwa na virusi hivyo.

Foleni katika mipaka ya TanzaniaHaki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Image captionTanzania bado haijafunga mipaka yake na Rais Magufuli ameahidi kutofanya hivyo

Wilaya ya Nakonde, inayopatikana kwenye mpaka wa Tanzania kusini ndiyo iliyoshuhudia visa vingi zaidi nchini Zambia ambapo ina zaidi ya nusu ya jumla ya visa vyote. Inazidi hata mji mkuu Lusaka.

Wilaya ya Nakonde ina kituo muhimu cha mpakani kinachotumiwa kusafirisha bidhaa na mizigo kutoka bandarini Tanzania hadi nchini Zambia.

Hali ni sawa upande wa Kenya – maafisa wamekuwa wakiwapima madereva kabla ya kuruhusiwa kuingia nchini humo.

Mwezi Mei pekee, zaidi ya raia 100 kutoka Tanzania wamegunduliwa kuwa na virusi hivyo baada ya kupimwa mpakani na kuzuia kuingia Kenya.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta alisema mnamo 16 Mei kwamba 29 waliokuwa wamezuru Tanzania wiki iliyotangulia walikuwa wamegunduliwa kuwa na virusi hivyo. Bw Kenyatta alifunga mpaka wa Kenya na Tanzania, ingawa malori ya kusafirisha mizigo yanaruhusiwa kupita

Katika vituo vya mpakani Uganda, madereva 15 wa malori kutoka Tanzania wamegunduliwa kuwa na virusi hivyo mwezi huu.

Wanawake sokoni TanzaniaHaki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Image captionSerikali ya Tanzania haijachukua hatua za kuwafungia watu

Shinikizo kwa serikali

Serikali imesema ina wasiwasi kwamba kuwafungia watu kunaweza kuwa na athari kubwa kwa maisha ya watu na uchumi, na pia hatua kama hiyo inaweza kuathiri sekta muhimu ya utalii.

Dkt Magufuli pia alitilia shaka usahihi wa matokeo ya vipimo vya corona vilivyokuwa vikifanywa na maabara ya taifa, baada ya sampuli za paipai na mbuzi kuonyesha zilikuwa na virusi.

Lakini baadhi wanaendelea kushangazwa na hatua za Dkt Magufuli na kutokuwa tayari kwake kufuata ushauri wa wataalamu wa afya kimataifa. (chanzo: BBC)