Ofisi ya Mufti yawapa mbinu kuepusha mifarakano masheikh Pemba

 

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

VIONGOZI wa dini ya kiislamu wa mkoa wa kusini Pemba, wametakiwa kutodhihirisha kwa wafuasi wao mahaba, upendo na kuvipigia chapuo vyama vyao vya siasa, wanapokuwa wanahubiri kwenye nyumba za ibada, kwani athari yake ni kusabisha mgawanyiko.

Ushauri huo umetolewa na Afisa Fat-tuwa na Utatuzi wa migogoro kutoka Ofisi ya Mufti Zanzibar, sheikh Thabiti Nouman Jongo, alipokuwa akizungumza na makhatibu, masheikh na viongozi wa dini ya kiislamu, ukumbi wa mikutano Baraza la mji Chake chake.

Alisema, iwapo viongozi hao watavitumia viriri vya miskiti kuelezea mahaba na utamu wa vyama vyao, waelewa kuwa huko ni kuwagawa waumini na kupelekea uvunjifu wa amani.

Alieleza kuwa, kazi yao kwa wafuasi wanaowagongoza ni kuelekeza namna ya kuishi kwa upendo, kudumisha amani na kuvumiliana na sio kuwaelezea mfumo wa vyama ulivyo.

Jongo alifahamisha kuwa, wajibu wao, ni kuona waumini wa dini ya kiislamu, hawagawanyiki na badala yake miskiti na madarasa mbali mbali, yawe yanajenga jamii moja.

“Ukijiona huwezi kuyazuaia mahaba ya chama chako, elewa kuwa hilo linaweza kusababisha migogoro na kisha kupekelea uvunjifu wa amani,’’alieleza.

Kwa upande wake Naibu Mufti wa Zanzibar sheikh Mahamoud Mussa Wadi, alisema siasa na uchaguzi ambao unakuja kila baada ya miaka mitano, usijaribu kuwagawa waislamu.

“Inawezekana kila kiongozi wa dini, kama walivyo wafuasi wetu tuna vyama vyetu, lakini hatupaswi kuwahubiria wengine maaa sisi tunakusanya makundi wenye vyama tofauti,’’alieleza.

Hivyo amewataka makhatibu hao, kuendelea kuandaa hutuba zenye mnasaba wa kuienzi na kuitunza amani, kwani ndio dira ya kutekeleza kila jambo kwa utulivu.

Mapema Katibu ofisi ya Mufti Zanzibar sheikh Khalid Ali Mfaume, alisema kwa njia yoyote ile, viongozi wa dini ndio wanaotegemewa kuwalainisha nyoyo kwa kutumia tafsiri za kur-an na hadithi.

Alisema uislamu daima umekuwa ukihimiza umoja, mshikamano, upendo na kukataza mgawanyiko kila siku, hivyo suala la mfumo wa vyama vingi, usiwe ndio muongozo wa waislamu.

“Isiwezekane hata kidogo kuwa, miongozo ya vyama vya siasa, katiba zao na kanuni yaje kugawa waislamu, kwani na sisi tunamiongozo yetu kama hadithi na kur-ani,’’alifafanua.

Akifungua mkutano huo wa siku moja, Mufti Mkuu wa Zanzibar sheikh Saleh Omar Kaabi, alisema umoja na mshikamano ndio silaha pekee ya kufikia malengo ya kuumbwa kwa mwanadamu.

Alisema, kwa vile dini ya kiislamu umekuja kuhimiza umoja hakuna mbadala wake, na ni wajibu wa kila muumini kuona hilo analitekeleza kwa vitendo.

“Siasa na uchaguzi ni mambo ya kupita, lakini mahaba na utii wa maamrisho ya Muumba, ndio ambayo yatakuwa daima na tukizipinda sheria zake, ni hasaraka kwetu,’’alieleza.

Hata hivyo amewakumbusha makhatibu hao, kuandaa hutuba zenye maudhui ya kuilinda na kuienzi amani iliyopo, ili kila kitu ikiwemo ibada ifanyike kwa utulivu wa hali ya juu.

Badhi ya viongozi hao wa dini, walisema wataendelea kuitunza amani iliyopo kwa kuwahubiria mema wafuasi wao, hata kama wanavyo vyama wanavyovipenda.

Khatib wa mskiti wa Mkoroshoni Chake Chake sheikh Said Abdalla Nassor, aliwashauri wenzake kuendelea kuhubiri amani, kwani zipo nchi kadhaa zilizoiharibu na sasa hawana maisha.

“Leo tembelea Sudan, Somalia, Yemen uone ambapo kila kitu hakifanyiki kwa utulivu ikiwemo ibada, hivyo lazima na sisi tuendelee na kuipigia chapuo amani yetu,’’alisema.

Nae sheikh Mohamed Khamis Mohamed wa Chake Chake, aliishauri ofisi ya Mufti kukutana na Tume ya Uchaguzi Zanzibar ‘ZEC’ kusitisha zoezi la upigaji kura, hadi nchi itakapotulia.

“Kila uchaguzi ukikaribia amani huchafuka na watu wasio na hatia kuvunjiwa heshima zao, sasa kwa hali ya nchi ilivyo, sio vibaya Tume ya Uchaguzi kwanza ikaghairisha upigaji kura hadi hapo baadae,’’alieleza.

Hata hivyo viongozi hao wa dini, wamesema wachafuzi wakubwa wa amani na wanaoanza viashiria vya uvunjifu wa amani ni baadhi ya viongozi wakuu wa vyama vya siasa.

Mwisho