Pemba hawajui eneo lililotengwa kwa wagonjwa wa Corona

 

IMEANDIKWA NA ZUHURA JUMA, PEMBA

WANANCHI kisiwani Pemba wameingiwa na hofu kutokana na kutojua sehemu maalumu ya kuwapeleka wageni wanaoingia pamoja na watu wengine wenye dalili za ugonjwa wa homa kali ya mapafu aina ya COVID-19 inayosababishwa na virusi vya Corona.

Walisema kuwa, hawaombi maradhi hayo kufika kisiwani hapa, ingawa wanahitaji kujua kituo maalumu kilichotengwa na Serikali, ili atakaejihisi na dalili za ugonjwa huo au mgeni kutoka nje ya nchi apate kukimbilia huko.

Wakizungumza na mwandishi wa habari kwa nyakati tofauti, walisema ipo haja kwa Wizara husika kuwajulisha wananchi eneo lililotengwa kwa ajili ya wagonjwa wa virusi vya Corona.

“Kujua kituo ni muhimu kwetu, kwani hadi sasa hatujui tukimbilie wapi iwapo mtu atajigundua na dalili za ugonjwa huu”, walisema wananchi.

Ali Hamad Shehe mkaazi wa Wingwi alisema kuwa, kwa vile kisiwa cha Unguja ilijitokeza kesi moja ya Corona, ni rahisi kwa Pemba kufika kutokana na muingiliano wa watu, hivyo ni vyema kikawekwa kituo maalumu ambacho wananchi watakijua.

“Hatuombi ugonjwa huu utufike, lakini inapotokezea mwananchi kaambukizwa aende wapi, wakati kwa Unguja limetengwa eneo la Kidimni lakini kwa Pemba sisi hatujui twende wapi”, alihoji mwananchi huyo.

Nae Hakima Ahmad Ali mkaazi wa Wete alieleza kuwa, kwa vile Zanzibar ni moja ni vyema kama iliyovyofanywa kisiwani Unguja na Pemba nao wakatangaziwa.

“Meli na vyombo vyengine vya usafiri kila siku vinakuja na kuondoka Pemba, sasa je akitokezea mtu ana dalili zote za Corona wapi hasa palipotengwa na Serikali aende”, aliuliza.

Asha Kombo Khamis mkaazi wa Chake Chake alisema, kutokana na ugonjwa huo ulivyo hatari ni vyema wakaelimishwa zaidi kupitia vipeperushi hasa, kwani wengine hawana radio wala televisheni, hivyo hawajui jinsi ya kujikinga wala unavyoambukiza.

“Pamoja na kuwa elimu inatolewa kwenye vyombo vya habari lakini kuna haja ya kutoa vipeperushi hata kwa kupitia angani, ili kuwafikia wananchi wote”, alisema mama huyo.

Kwa upande wake Ali Hamad Salum mkaazi wa Msingini Chake Chake alisema kuwa, ugonjwa wa Corona unaenea kwa kasi hivyo ni vyema kutolewe elimu ya kujikinga sambamba na kuwajuza sehemu iliyotekwa kwa ajili ya wagonjwa hao, ili iwe rahisi.

“Kama atatokezea mtu ana dalili ya ugonjwa huo kwa kweli hajui akimbilie wapi, maana hatujaambiwa kuwa sehemu fulani ndio iliyotengwa, mtu atahangaika, jambo ambalo linaweza kusababisha madhara zaidi”, alisema.

Afisa Mdhamini Wizara ya Afya Pemba Shadya Shaaban Seif alisema, kwa sasa hakuna sehemu maalumu iliyotengwa kwa ajili ya wagonjwa hao na kuwataka wananchi kukimbilia haraka hospitali kuu za Serikali wanapojihisi na dalili hizo.

Alisema, si vyema wananchi kuwaacha majumbani watu wenye dalili za ugonjwa huo na badala yake wakimbilie hospitali, huku Serikali ikiendelea na jitihada zake kutayarisha eneo rasmi kwa ajili ya wagonjwa watakagundulika na maambukizi ya Covid-19 (Corona).

“Hospitali zote za Wilaya na Mkoa mtu anaejihisi na dalili za Corona anatakiwa aende kutafuta matibabu, hapo atachukuliwa vipimo vyake na kusafirishwa kwa ajili ya uchunguzi”, alisema Afisa huyo.

Shadya aliomba jamii kutoa ushirikiano mkubwa kwa kufuata maelekezo na taratibu za kujikinga na kufuata kanuni za afya hasa kunawa mikono mara kwa mara.

Aidha aliwataka wanajamii kutoa taarifa endapo ameingia mgeni kutoka nje ya nchi, ili Wizara iweze kumfuatilia na kujulikana afya yake, ili asije kuangamiza jamii endapo ana maambukizi ya ugonjwa huo.

Machi 22 mwaka huu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli ametangaza kuwa nchi hiyo ina wagonjwa 12 walioambukizwa ugonjwa wa corona, ambapo wanane kati ya wagonjwa hao ni raia wa Tanzania na wengine wanne ni raia wa kigeni.

Wakati huo huo Shirika la Afya Duniani (WHO) liliutangaza ugonjwa wa Covid-19 kuwa dharura ya kimataifa (Global Health Emergency), na tayari shirika hilo kuanzia Machi 11 mwaka huu iliutangaza kuwa janga la kimataifa.

 

MWISHO.