‘SWIOFish’ mradi unaobadili maisha endelevu ya wavuvi Zanzibar’

 

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

MTAALAMU wa mawasiliano kwenye Mradi wa Usimamizi wa Uvuvi Kanda ya Kusini Magharibi mwa bahari ya Hindi ‘SWIOFish’  Zanzibar Ali Sultan, amesema mradi huo, umeshazaa matunda kwa wavuvi na walaji, ikiwa ni uwepo wa uvuvi wa uhakika wa samaki jamii ya pweza.

Alisema, ushahidi wa maeneo hayo ni pamoja na shehia za Kilindi, Kukuu, Pujini na Fundo kisiwani humo, ambapo sasa wavuvi wa maeneo hayo, wamekuwa wakivua pweza wenye uzito kati ya kilo tano hadi sita.

Mtaalamu huyo wa Mawasiliano, alikuwa kizungumza na waandishi wa habari na wasanii kwenye ukumbi wa Idara ya Nyaraka Chake Chake, kwenye kikao cha kubuni njia za kuwafikishia taalamu ya uvuvi, wavuvi na wananchi kisiwani Pemba.

Alisema mradi huo wa ‘SWIOFish’ ambao lengo hasa ni kutoa taaluma na kufanya utafiti, umekuwa kigezo kikubwa kwa wavuvi wa ndani na nje kwa kule kuimarisha na kukuza pato la wavuvi mmoja mmoja na taifa.

Sultan alieleza kuwa, maeneo kama ya shehia ya Kukuu wilaya ya Mkoani, wapo wavuvi kutoka Lindi, Lamu na Mtwara wameshafika kwa ajili ya kujifunza namna wenzao walivyofanya na kuwa na uvuvi wa pweza wenye tija.

Alisema, alipozungumza na wavuvi wa shehia hiyo, walithibitisha kuwa mradi huo kwa sasa, unawapatia pweza wakubwa jambo ambalo halikuwepo kwa miaka zaidi ya 30 iliopita.

“Wavuvi sasa wanakiri kuwa wanavua pweza wenye uzito wa katia ya kilo tano hadi sita, ambapo kabla ya mradi huu ambao ulipelekea baadhi ya maeneo kuhifadhiwa, walikuwa wakivua wajukuu wa pweza,’’alieleza.

Hivyo amewataka waandishi wa habari kuwafuata wavuvi hao na kuwahoji na kisha kuandika makala na vipindi ambavyo, vitawapa mwanga wavuvi na wananchi wengine wa ukanda wa bahari, kuanzisha uhifadhi shirikishi.

Katika hatua nyingine, Mtaalamu huyo wa Mawasiliano alisema, sehemu pia ya mradi huo ni kufanya sensa ya uvuvi na wavuvi, ili kujua changamoto na mbinu za kukuza uchumi wa taifa kupitia ‘blue economy’.

Kwa upande wake Mratibu wa mradi wa huo kisiwani Pemba, Ali Kassim Mohamed, alisema mradi huo hasa umejikitia katika mambo matano, ingawa kwa Zanzibar uko kwenye maeneo matatu.

“Moja ni kuhifadhi aina ya samaki jamii ya wanaoelea ‘small pelagic’ wakiwemo dagaa na vibua, samaki wa miambani ‘rick fish’ pamoja na jamii ya samaki aina ya pweza,’’alieleza.

Alisema kwa hatua za awali mradi huo, uko kwenye shahia 10 ikiwa ni pamoja na Makombeni, Mizingani, Wambaa, Kilindi, Mgelema, Tibirinzi, Chonga, Wesha, Ndagoni na Shungi ambapo wavuvi wamshajengewe uwelewa.

Mratibu huyo alieleza kuwa, shehia hizo ni za majaribio kwa muda wa mwaka mmoja, na kuanzia mwezi Julai mwaka 2020, kutakuwa na shehia nyingine ambazo zitaingia kwenye mradi huo.

“Kwa shehia hizo kwanza, tulianza na uchaguzi wa kamati za watu 10 za shehia, ambapo kila mvuvi anawakilisha kundi la wavuvi wa aina ya uvuvi fulani,’’alifafanua.

Alisema, baada ya hapo sasa wameshawapa taaluma ya usimamizi shirikishi wa shughuli za uvuvi, katika shehia zao na kuzitambua rasilimali zilizopo katika maeneo yao.

“Lengo baada ya kugundua kuwa miradi iliopita kwamba shehia moja inahifadhi na nyengine inavamia, sasa kupitia mradi huu wa ‘SWIOFish’ kutakuwa na ulinzi shirikishi miongoni mwa shahi hizo,’’alieleza Mratibu huyo.

Baadhi ya waandishi wa habari waliohudhuria mkutano huo, walisema bado wanahofu juu ya miradi kama hiyo, kwamba inapomalizika walengwa hurudi kwenye maisha ya kufukuzana.

Mwandishi wa shirika la magazeti ya serikali Pemba Bakari Mussa Juma, alisema serikali hupokea miradi ya muda mrefu kama ya MACEMP na yenye thamani na inapomalizika wavuvi hurudi tena kwenye uvuvi wa kubahatisha.

“Mimi nataka kujua kupitia mradi huu wa zaidi ya miaka 14, Idara ya maendeleo ya uvuvi imejipanga vipi, kuhakikisha wavuvi wetu hata baada ya mradi, wanavua pweza wenye kilo tano hadi sita,’’aliuliza.

Nae mwandishi na mtangazaji wa Shirika la Utangazaji Zanzibar ‘ZBC’ Mchanga Haroub Shehe, alisema ni jambo jema kupitia mradi huo, ambao hauwanufaisha wavuvi pekee, bali hata wananchi wote.

“Mimi nilitembelea shehia ya Kilindi, kuzungumza na wavuvi na wananchi, wamenionyesha matunda ya mradi huu wa ‘SWIOFish’ maana sasa wameshajenga madarasa ya kusomea, kutokana na faida ya uhifadhi na kisha kuvua kwa uhakika,’’alieleza.

Wakati huo huo Afisa habari na mawasiliano kutoka Idara ya maendeleo ya uvuvi Zanzibar Semeni Mohamed Salum, alisema, ujio wa mradi huo ni baada ya benki ya dunia kuridhishwa na utekelezaji wa mradi wa MACEMP.

Alisema mradi wa MACEMP ambao ulifanya kazi kwenye vijiji zaidi ya 400,  na kutumia wastani wa shilingi milioni 10 hadi 15 kwa kijiji mimoja, ndio uliozaa matunda na wafadhili kuvutika hadi kuuletwa mradi wa SWIOFish wa miaka 15.

Mradi wa Usimamizi wa Uvuvi Kanda ya Kusini Magharibi mwa bahari ya Hindi ‘SWIOFish, kwa sasa unatekelezwa kwenye nchi za Mozambique, Comoro na Tanzania Zanzibar pekee.

Ambapo kwa Unguja mradi huu utatekelezwa kwenye eneo la hifadhi ya ‘MENAI’ na eneo la hifadhi ya Mnemba MNEMBA, na Pemba ni PECCA, ambapo utakuwa ni mpango miaka 15, ulioanzia mwaka 2015 na kumalizika mwakani kwa hatua ya kwanza.

mwisho