TAMWA yatoa rai kwa wanahabari Pemba kumaliza udhalilishaji

 

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania ‘TAMWA’ ofisi ya Zanzibar, kimewataka waandishi wa habari wanaoandika habari za udhalilishaji na ukatili wa kijinsia, kwa wanawake na watoto, kujenga utamaduni wa kuzifuatilia mwanzo hadi mwisho habari hizo, ili jamii ijue namna zilivyoishia kama zilivyoanzia.

Rai hiyo imetolewa na Afisa Ufuatiliani na tathimini kutoka TAMWA Zanzibar, Mohamed Khatib Mohamed, alipokutana na waandishi wa habari, wanaoandika habari hizo kisiwani Pemba, kwenye ofisi za TAMWA Chakechake Pemba, juu ya kutafuta mbinu ya kumaliza udhalilishaji huo.

Alisema, njia moja nzuri ya kujenga ushirikiano katika kumaliza udhalilishaji unaowaandama wanawake na watoto, ni vyema kwa waandishi wa habari, nguvu wanayoitumia kuliripoti tukio la udhalilishaji kwa mara ya kwanza, waiendeleze kwa siku za mbele.

Alisema imekuwa ni kawaida, kwa baadhi ya waandishi kuwaripotia wananchi juu ya mtu fulani kumbaka au kumlawiti mtoto, na kisha mtuhumiwa huyo akishafikishwa mahakamani hakuna habria nyingne inayoandikwa.

Alisema, ili kuwe na ufuatiliaji nzuri na jamii iweze kupata tathmini nzuri juu ya kazi za waandishi wa habari, ni vyema matukio wanayoaanza kuyaripoti awali, kisha waendelee kuripoti kwa kila hatua ya kesi husika.

“Pengine waandishi kupitia vyombo vyenu, mmekuwa na hamasa kubwa kusikia tukio sehemu mkaenda kwa wingi, lakini mtuhumiwa akishapandishwa mahakamani hatusikii tena habari, sasa hapa huwa tunakosa muendelezo wa tukio lilipofikia,’’alifafanua.

Hata hivyo katika hatua nyingine, Afisa huyo ufuatiliaji na tathmini kutoka TAMWA Zanzibar, aliwataka waandishi kutoegemea kwenye kuripoti habari za aina za ina moja za udhalilishaji, kama ubakaji na ulawiti na kuacha maeneo mengine.

Alisema udhalilishaji kama wa utoroshaji, utelekezaji, kujaribu kubaka, kujaribu kulawiti, kumfinya mtoto bado kumekuwa na kasi ndogo kwa vyombo vya habari, kuripoti eneo hilo.

Mapema Mratibu wa TAMWA Pemba Fat-hiya Mussa Said alisema, nguvu ya pamoja ya vyombo vya habari, ndio njia pekee, inayoweza kumaliza vita vya udhalilishaji na ukatili kwa wanawake na watoto.

Alisema, kazi inayofanywa na waandishi wa habari bado inahitaji kuongezewa nguvu, ili kuona kila linapotokezea kumekuwa na vyombo vinavyoripoti kwa pamoja.

“Kazi mnayofanya ni kubwa, lakini bado mnatakiwa kwa kushirikiana na wadau muongeze nguvu, maana nao wadhalilishaji ndio kwanza wanachipukia ndani ya jamii yetu,’’alieleza.

Kwa upande wake, mwandishi na mtangazaji wa shirika la utangaazaji ‘ZBC’ Pemba, Khadija Kombo Khamis alisema lazima waandishi washirikiane kikamilifu, katika kufuatilia matukio hayo.

Nae mwakilishi wa ITV/redio One Suleiman Rashid Omar, alisema ipo haja kwa TAMWA, kuwaunga mkono waandishi wa habari wanaoonesha moyo wa kuandika habari za aina hiyo.

“Inawezekana wapo waandishi wamekuwa woga kuripoti kwa kina habari hizi, lakini kwa wale ambao wameshakubali kujitolea kuziandika, basi waengwe engwe na TAMWA, ikiwa ni pamoja na kuwapa motisha,’’alifafanua.

Hata hivyo mwandishi Tif tv Pemba, Abdalla Amour, alisema ni vyema kwa TAMWA, ikiwawezesha kimafunzo zaidi waandishi wa habari wachanga, ili wafahamu vyema namna ya kuandika habari hizo kama walivyowengine.

Katika siku za hivi karibuni matukio ya udhalilishaji yamekuwa yakiongezeka kwa kasi, hali inayopa hofu wanaharakati, serikali na jamii kwa ujumla.

                                    Mwisho