TAMWA-Zanzibar, ACTION AID wachanga nguvu kupambana na udhalilishaji

 

IMEANDIKWA NA Muhammed Khamis, Tamwa-Zanzibar

CHAMA cha Waandishi wa  Habari Wanawake TAMWA -Zaizibar kwa kushirikiana na shirika la Action Aid katika  lengo la kupambana na udhalilishaji wa kijinsi, wamewapatia mafunzo wanajamii 660 kutoka shehia 22 Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja.

Afisa wa masuala ya udhalilishaji kutoka TAMWA-Zanzibar Zaina Salum Abdaala alisema lengo kuu la mafunzo hayo kwa wanajamii hususani wanawake ni kujengewa ufahamu zaidi juu ya  dhana nzima  ya udhalilishaji na  madhara yake kwa kuwa bila ya kuwa na elimu sahihi dhidi ya matendo hayo hayataweza kumalizika.

Alieleza kuwa, anaamini  elimu hio ilitolewa kwa muda wa wiki mbili  kwa wanajamii italeta mabadiliko makubwa
ikiwemo wanajamii kufahamu viashiria vya udhalilishaji sambamba na umuhimu wa kutoa taarifa mara pale matukio hayo yanapojitokeza kwenye jamii.

Alisema kuwa katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar hadi sasa baadhi ya wanajamii wamekua wakiyafumbia macho matendo  hayo  kwa wanawake na watoto kutokana  kuhofia sababu mbali mbali ikiwemo kuvunjika kwa ndoa zao.

‘’Kuna matukio mbali mbali ya udhalilishaji yanafanyika lakini watu wapo tayari kuona yanaendela  lakini hushindwa kusema kwa kuhofia kupewa talaka na waume zao’’aliongezea.

Hata hivyo Afisa huyo  aliasa jamii i kubadilika na kutokua na muhali badala yake watoke na kutoa
taarifa dhidi ya matendo hayo kwa lengo la kuchukuliwa hatua kali zaidi kwa watendaji wote watakaobainika kutenda unyama huo.

Akizungumza kwa niaba ya Masheha wenzake sheha wa shehia ya Kitope Khamis Ndende Juma alisema ni kweli
kuwa wamekua wakikabiliwa na matukio mbali mbali ya udhalilishaji kwenye jamii zao kiasi cha kwamba walio wengi wameanza kushtuka na kuhofia madhara zaidi.

Alisema sula la muhali  bado ni tatizo ambalo wanaendelea kukabiliana nalo ndani ya jamii zao kwa kuwa  wapo baadhi ya watu wanatendewa matendo hayo na kisha kuamua kunyamaza kimya.

Hata hivyo Sheha huyo  alisema kupitia elimu hio ilitolewa na TAMWA-Zanzibar anaamini kwa kiasi kikubwa atakwenda kubadili jamii na hatimae watu kuwa tayari kutoa ushirikiano wa kina dhidi ya matendo hayo kwa lengo la kuyamaliza kabisa.

Mzee Ali Makame kutoka  shehia ya Kitope alisema ili jamii iweze kumaliza tatizo hilo ipo haja kuhakikisha wazazi na walezi wanakua karibu zaidi na watoto wao kila wakati.

Alisema baadhi ya matukio mengi yanayotokea yanaonesha wazi kuwa baadhi ya wazazi ama walenzi  wamekosa umakini katika suala zima la uangalifu kwa watoto na wakati mwengine hua sababu ya kufanyiwa unyama huo.

Kwa upade wake Afisa  Dawati la Jinsia Mkoa wa kaskazini Unguja Salum Khamis Machano alisema jeshi la
polisi kupitia dawati la jinsia  wanajitahidi  kwa kiasi kikubwa kupambana na matukio hayo ikiwemo kuwachukulia hatua wale wote wanaofikishwa katika dawati hilo.

Hata hivyo Afisa huyo  alisema bado kuna tatizo ndani ya jamii ikiwemo la kukosa utayari wa kuendelea  na baadhi ya kesi ambazo huwa tayari zimeshafikishwa katika vituo mbali mbali vya polisi.

Aliomba jamii kubadilika  na kuyachukuliwa matendo hayo kuwa ni ya kinyama na yasiopaswa kuvumiliwa kwa
mtu yoyote yule awe mzee,mtoto ndugu au jirani

mwisho