TAMWA-Zanzibar yawaelekeza wajasiriamali kutumia karafuu kwa uzalishaji wa bidhaa

 

IMEANDKWA NA MUHAMMED KHAMIS-TAMWA-Zanzibar

MKURUGENZI wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake TAMWA- Zanzibar Dk, Mzuri Issa amewataka wajasiriamali wanawake kisiwani Pemba kutumia vizuri neema ya zao la karafuu kwa  kuzalisha bidhaa mbali mbali.

Dk Mzuri aliyasema hayo leo Juni 26, mwaka huu wakati alipokua akizikagua baadhi ya bidhaa zinazozalishwa na wajasirimaali kutoka Pemba ofisini kwake Tunguu Wilaya ya kati Unguja.

Alisema, zao la karafuu linaweza kuzalisha bidhaa mbali mbali ambazo zina soko kubwa ndani na nje ya nchi iwapo wajasiriamali hao wataweza kuzisanifu vyema karafuu hizo.

Akitolea mfano wa bidhaa zinazotokana na karafuu alisema, ni sabuni pamoja na liwa ambalo ni maalumu kutumika kwa ajili ya kusafishia mwili kwa wanawake na wanaume.

Pia Mzuri aliwataka wajasiriamali hao kuanza kuangaza zaidi soko la kimataifa ambapo pia kuna uhitaji mkubwa wa bidhaa za asili kutoka Zanzibar, hususani zinazoalishwa kwa kutumia bidhaa ya karafuu.

Kwa upande wake Afisa Uwezeshaji Wanawake TAMWA ofisi ya Pemba Asha Mussa Omar alisema, wanawake wengi kisiwa cha Pemba wamehamasika kujiunga kwenye vikundi mbali mbali vya uzalishaji wa bidhaa.

Akitolea mfano alisema, pia wajasiriamali hao hawakuridhika tu na uzalishaji wa bidhaa hizo pia wameanza kujiingiza katika ufuagaji, ambapo tayari baadhi ya vikundi vinamiliki mabanda na wanaendelea na ufugaji kuku.

Akizungumzia kuhusu changamoto alisema bado zipo ikiwemo ukosefu wa soko la uhakika kwa wajasiriamali ambapo wakati mwengine hulazimika kukaa na bidhaa zao ndani kwa muda mrefu.

Afisa huyo aliiomba Serikali na taasisi nyengine mbali mbali kujitokeza kwa wingi kuunga mkono jitihada za vikundi hivyo kwani kufanya hivyo kutawawezesha wanawake wengi kujikwamua kiuchumi na kuondokana na umasikini.

Akizungumzia kuhusu hali halisi ya uzalishaji wa bidhaa, mmoja wa wajasiriamali kutoka kisiwani Pemba Sakina Ame Bakar alisema, wanajitahidi kuzalisha bidhaa  bora na zenye viwango vya hali ya juu.

Alisema licha ya jitihada hizo lakini wanaendelea kukabiliwa na changamoto ya ukosefu wa soko la uhakika ambalo lingewafanya wajasiriamali kuwa bora na wakimataifa.

Aidha aliomba Serikali kuendelea kuwatengezea mazingira bora ikiwemo kuwakutanisha na makampuni makubwa pamoja na wajasiamali wengine wa kimataifa ili waweze kutengeza masoko mapya.