Trump: Shirika la Afya liko chini ya ‘Udhibiti wa China’

 

Rais Donald Trump hatimaye ametoa notisi ya kujiondoa kwa Marekani katika shirika la Afya Duniani WHO.

Rais huyo aliweka wazi lengo lake mwezi Mei , akililaumu shirika hilo la WHO kuwa chini ya udhibiti wa China kufuatia mlipuko wa virusi vya corona.

Licha ya wito kutoka kwa Muungano wa Ulaya na wengine, alisema kwamba ataiondoa Marekani kutoka katika kitengo hicho cha UMoja wa Mataifa UN na kupeleka ufadhili wake kwengineko.

Kufikia sasa ametoa ilani kwa UN na bunge la Congress kuhusu malengo yake, ijapokuwa mkakati huo unaweza kuchukua kipindi cha mwaka mmoja.

Stephane Dujarric, msemaji wa katibu mkuu wa UN, alithibitisha kwamba Marekani imetoa ilani kuhusu kujindoa kwake kuanzia tarehe 6 Julai 2021.

Seneta Robert Mendez , kiongozi wa Democrat katika kamati ya masuala ya kigeni, pia aliandika katika twitter: Congress imepokea notisi kwamba POTUS {rais wa Marekani} amejiondoa rasmi katika shirika la Afya Duniani WHO katikati ya mlipuko wa corona.

”Inaiwacha Marekani ikiugua na pekee”

Afisa mkuu wa utawala wa rais Trump aliambia CBS News kwamba Washington ilielezea mabadiliko inayohitaji WHO kufanya na kujadiliana nayo moja kwa moja , lakini Shirika hilo limekataa kuchukua hatua.

“Kwasababu wamefeli kufanya mabadiliko yaliotakiwa , hii leo tutavunja uhusiano wetu , afisa huyo alinukuliwa akisema.

Joe Biden, ambaye atampinga rais Donald Trump katika uchaguzi wa mwezi Novemba , alituma ujumbe wa Twitter akisema: Katika siku ya kwanza kama rais, Nitairudisha Marekani katika WHO na kuimarisha uongozi wetu duniani.

Marekani ndio mfadhili mkuu wa shirika hilo, likitoa $400m (£324m; €360m) mwaka 2019, takriban asilimia 15% ya bajeti yake kwa jumla.

Chini ya uamuzi wa Congress 1948, Marekani inaweza kujiondoa lakini lazima itoe notisi ya mwaka mmoja na italazimika kulipa fedha inazodaiwa , ijapokuwa haijulikani ni upi msimamo wa Trump kuhusu hilo.

Bwana Dujarric alisisitiza kuwa masharti hayo ni lazima yaafikiwe. Kujiondoa huko kutagusia uwezo wa kifedha wa shirika hilo na hatma ya mipango yake kukuza afya na kukabiliana na magonjwa.

Ni nini alichosema rais Trump kuhusu WHO?

Mara ya kwanza alitangaza mwezi Aprili kwamba atasitisha ufadhili wa Marekani kwa shirika hilo hadi pale litakapojirekebisha katika kipindi cha siku 30.

Baadaye Mwezi Mei alisema: Tutavunjilia mbali uhusiano wetu na kuagiza ufadhili wetu kwenda kusaidia afya katika mashirika ya hisani duniani.

Ulimwengu sasa unapata tabu kutokana na utapeli uliofanywa na serikali ya China, alisema akiongezea kwamba China ilisababisha janga duniani.

Rais huuyo aliishutumu China kwa kuishinikiza WHO kudanganya ulimwengu kuhusu virusi hivuo, bila ya kutoa ushahidi kuhusu madai yake.

China udhibiti mkubwa katika shirika la afya Duniani, alisema rais huyo.

Mataifa mengine , ikiwemo Ujerumani na Uingereza , yamesema hayana lengo la kutaka kujiondoa kutoka kwa shirika hilo, ambalo linasimamia mpango wa kupata chanjo ya virusi vya Covid-19.

Je WHO ni nini – na nani anayelifadhili?

  • Likianzishwa 1948 na makao yake yakiwa mjini Geneva, nchini Switzerland, ni kitengo cha Umoja wa mataifa kinachosimamia Afya duniani.
  • Shirika hilo lina mataifa wanachama 194 na lengo lake ni kukuza Afya, kuhakikisha dunia iko salama na kuwahudumia wasiojiweza.
  • Likihusishwa na kampeni za chanjo, afya za dharura na kusaidia mataifa mbali na kutoa uangalizi wa mapema
  • Linafadhiliwa na muungano wa wanachama kulingana na uwezo na idadi mbali na ufadhili wa kujitolea. (bbc)