Uchunguzi haujakamilika hadi lini ?

Imeandikwa na Salmin Juma – Zanzibar

Email:salminjsalmin@gmail.com

Chama cha Waandishi wa habari wanawake Tanzania TAMWA upande wa Zanzibar kimatakiwa kupendekeza katika utafiti wao, kuchunguzwa utendaji kazi kwa baadhi ya askari Polisi wapelelezi wa kesi za udhalilishaji wa kijinsia,  kwakua kesi nyingi zinazoripotiwa zinachukua muda mrefu mikononi mwao wakidai kua uchunguzi haujakamilika hali ambayo inawafanya wadai wa kesi hizo kukata tamaa na wengine kupoteza imani na kesi hizo.

Mapendekezo hayo yalitolewa juzi na mwandishi wa habari ambae hakupenda jina lake lichapishwe mtandaoni,  katika mkutano maalum uliyoitishwa na chama hicho huko Tunguu Unguja, uliyokua na lengo la kupokea maoni  na ushauri katika ripoti iliyobeba ujumbe wa “vitendo vya udhalilishaji” kupitia utafuti uliyofanyika katika wilaya ya Kaskazini “A” Unguja na wilaya ya mkoani Pemba 2019.

Akizungumza mbele ya hadhara ya watu wa makundi tofauti wakiwamo wanaharakati wa kupinga udhalilishaji, mwandishi huyo alisema, kutokana na utafiti ulivyoonesha kuwa kesi nyingi za udhalilishaji bado zipo mikononi mwa Polisi kwa kua hazijakamilika upelelezi wake, ni kheri kupitishwe mapendekezo katika ripoti hiyo ya kuwepo sheria itakayo wafanya askari kupimwa utendaji wao kupitia kesi hizo.

“lakini pia ripoti ipendekeze, ifanywe kuwa ni kosa kutokwenda kutoa ushahidi mahakamani, pamoja na kufungua kesi kisha kutoimaliza, kwani huko ni kuwafanya watu kama hawana kazi za kufanya” alisema mwandishi huyo.

Nae Ali Sultan mwandishi mkongwe visiwani Zanzibar, alitilia mkazo suala hilo kwa kusema kuwa, nchi zenye vita duniani kama vile, Congo, Darfur, na hata huko Iraq, bado hawajafikia kiwango kikubwa cha ubakaji kama inavyoshuhudiwa hapa Zanzibar, wakati huko ndiko kwenye uwezekano mkubwa wa kutokea hayo kwakua kuna vita vinavyoendelea kila leo.

Pia alisema ni lazima kuangaliwe kwa kina kuhusu madai ya Polisi kuwa uchanguzi haujamilika katika matukio hayo “ kuwekwe limit ya kuzimaliza hiki kesi, uchunguzi hadi lini” alisema Sultan

Kwa upande wake Ali Haji Mwadini, mshauri mwelekezi, alipokua akiwasilisha ripoti hiyo kwa niyaba ya TAMWA alisema, vitendo vya udhalilishaji katika wilaya hizo vinaonekana kushamiri huku kesi nyingi hazijapatiwa hukumu zipo mikononi mwa jeshi la polisi.

“Kutoka Januari hadi Oktoba Wilaya ya kaskazini “A” kumeripotiwa kesi za ubakaji 43 na wilaya ya Mkoani Pemba kesi 45” alisema mwadini.

Awali akifungua mkutano huo, Kaimu Mkurugenzi wa Tamwa upande wa Zanzibar Bi Asha Abdi alisema, kwa kutambua umuhimu wa wadau katika mapambano ya vita dhidi ya udhalilishaji, ndio wakaamua kuwapa nafasi ya kutoa maoni juu ya utafiti huo na ripoti iliyofanyika ili kuongeza au kupunguza jambo kwa lengo la kuiboresha.

Alisema, kutokana na ukubwa wa tatizo, inawapasa wanawake wanapokutana wahimizane kuzisimamia kesi hizo pamoja na kuondosha muhali kwani wahanga wakubwa ni wao.

“wanawake hata tunapokua mashuhulini tuambizane wenyewe kwa wenyewe tuache muhali ili mambo yaende” alisema Abdi.

Mkutano huo umewakutanisha wadau mbalimbali nchini, wakiwamo waandishi wa habari, wanaharakati wa kidini na wakawaida, wanasheria na wengineo.