Upande wa mashitaka Pemba wakubali hoja za upande wa utetezi

 

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

UPANDE wa Mashtaka, umekubali ushauri wa upande wa utetezi uliokuwa ukiongozwa na wakili Ali Hamad, kuwa waendelee na kesi ya msingi, badala ya kusubiri uamuzi mdogo wa mahakama, katika shauri la kupatikana na vicha 12 vinavyoaminika kuwa ni vya dawa za kulevya.

Awali mara baada ya kuwasili mtuhumiwa mahakama hapo akisimamiwa na wakili wake, Hakimu wa mahkama ya mkoa ‘B’ Chake Chake Luciano Makoye Nyengo, aliuuliza upande wa mashitaka juu ya hatua ya kesi hiyo.

Wakili wa serikali kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa mashtaka Ramadhan Suleiman Ramadhan alidai kuwa, shauri hilo lipo kwa ajili ya kutajwa, ingawa kuna hoja za uamuzi hazijajibiwa.

Alidai kuwa, kutokana na hali hiyo, waliweka nia ya kutaka kuzikatia rufaa hoja zilizowasilishwa, na kuiomba mahakama kuliahrisha shauri hilo na kulipangia tarehe nyingine.

“Mheshimiwa shauri lipo kwa ajili ya kutajwa, lakini kuna hoja na sisi tulitaka kuzikatia rufaa, sasa ni vyema ukaliahairisha na kulipangia tarehe nyingine,’’alidai wakili huyo wa serikali.

Mara baada ya maelezo hayo, Hakimu Luciano Makoye Nyengo, aliiuliza upande wa utetezi ikiwa wameziskia hoja za upande wa mashitaka wanaotaka kwanza, usubiriwe uamuzi mdogo wa mahkama.

Wakili wa utetezi katika shauri hilo la kupatikana na vicha 12 vinavyoaminika kuwa ni vya dawa za kulevya Ali Hamad, aliimbia mahakama hiyo kuwa, kwanza na wao ilitakiwa wapewe notisi ya uamuzi huo.

“Kisheria ilipaswa ipelekwe na kurejeshwa sio zaidi ya siku 14 na kisha sisi tupewe, lakini sasa ni muda mrefu umeshapita hatujapewa, hivyo ni vyema Mheshimiwa tungaliendelea na shauri lilipofikia,’’alipendekeza.

Aidha wakili huyo wa utetezi aliomba mahakama hiyo, kuendelea na hatua ya kesi ya msingi ilipofikia, kwa vile hakuna kinachoathirika wakati ikiendelea.

Hivyo hakimu huyo mara baada ya kusikiliza hoja za pande mbili hizo, ambapo upande wa mashtaka ulikubaliana na hoja ya upande wa utetezi, aliliahirisha shauri hilo Febuari 6, mwaka huu.

Awali ilidaiwa mahkamani hapo kuwa, mtuhumiwa huyo bila ya halali alipatikana na vicha 12 vya majani mabichi yanayoaminika kuwa ni ya dawa ya kulevya, aina ya mirungi yenye uzito wa gramu 1,140 jambo ambalo ni kosa kisheria.

Tukio hilo lilidaiwa kutokea Julai 15 mwaka juzi majira ya saa 11:10 jioni eneo la uwanja wa Ndege wilaya ya Chake Chake, ambapo ni kinyume na kifungu cha 13 (d) cha sheria ya udhibiti wa dawa za kulevya, sheria namba 9 ya mwaka 2009.

Aidha pia ni kosa kisheria kukamatwa na mirungi, kama ilivyofanyiwa marekebisho na sheria namba 12 ya mwaka 2011 sheria Zanzibar.

Mwisho