Vikosi vya Haftar vyaua watu 40 katika sherehe ya harusi nchini Libya

Watu wasiopungua 40 wameripotiwa kuuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa baada ya shambulio la anga lililofanywa na vikosi vya Jenerali Khalifa Haftar vinavyojiita Jeshi la Taifa la Libya kulenga sherehe ya harusi kusini magharibi mwa nchi hiyo.

Vyombo vya habari vimeripoti kuwa, shambulio hilo la ndege isiyo na rubani ya droni liliwalenga watu waliokuwa kwenye sherehe ya harusi iliyofanyika katika mji wa Murzuq hapo jana.

Karibu watu 1,100 wameripotiwa kuuawa tangu vikosi vya Haftar vyenye makao yao mashariki mwa Libya vilipoanzisha hujuma na mashambulio dhidi ya mji mkuu wa nchi hiyo Tripoli Aprili 4 mwaka huu.

Duru za serikali ya Libya inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa ziliripoti hapo kabla kuwa, makumi ya watu waliuawa pia katika shambulio la anga lililofanywa na vikosi vitiifu kwa Haftar dhidi ya kambi ya wakimbizi iliyoko mjini Tripoli.

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya Ghassan Salame amependekeza usitishaji vita kwa heshima ya Sikukuu ya Idul-Adhha inayotazamiwa kusherehekewa na Waislamu kote dunaini siku ya Jumapili au Jumatatu ijayo na vile vile amezitaka pande hasimu kuanzisha tena mazungumzo baina yao.

Umoja wa Ulaya pia ulitoa taarifa siku ya Ijumaa kuzitaka pande zinazopigana nchini Libya kutekeleza usitishaji vita wa kudumu na kurudi kwenye meza ya mazungumzo yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi.

Tangu baada ya mapinduzi ya wananchi ya mwaka 2011 yaliyouangusha utawala wa Muammar Gaddafi kwa uingiliaji wa Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya na za eneo, Libya imepoteza uthabiti wa kisiasa na kuwa uwanja wa mapigano na machafuko ya wenyewe kwa wenyewe.

Kwa mwaka wa nne sasa nchi hiyo imekuwa na tawala mbili, mmoja ukiwa ni wa bunge lenye makao yake katika mji wa mashariki wa Tobruk likiungwa mkono na vikosi vya jeshi la taifa la Libya vinavyoongozwa na Jenerali Khalifa Haftar na mwengine wa serikali inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa inayoongozwa na Waziri Mkuu Fayez al-Sarraj, ambayo makao yake yako mji mkuu wa nchi hiyo, Tripoli.

Vikosi vya Haftar vinaungwa mkono na Saudi Arabia, Misri, Imarati na baadhi ya nchi za Magharibi.