Wabunge wanawake wapigwa ‘stop’ kusafiri nje ya nchi

 

Israel imeamua kuwawekea vikwazo vya usafiri wabunge wawili wa chama cha Democratic nchini Marekani baada ya Rais Trump kuiomba nchi hiyo kuwapiga marufuku

Bwana Trump alisema “itaonesha udhaifu mkubwa” ikiwa Israel itawaruhusu Ilhan Omar na Rashida Tlaib kuzuru taifa hilo.

Hatua hiyo inakuja baada ya tamko la balozi wa Israel nchini Marekani mwezi uliopita kuwa wawili hao wataruhusiwa kuingia nchi hiyo.

Israel imekua ikiwapiga marufuku wafuasi wa vugu vugu linalosusia taifa hilo, kitu ambacho viongozi hao wawili wanaunga mkono.

Hatua huyo imethibitishwa katika taarifa iliyotolewa na wazara ya mambo ya ndani ya Israeli, ambayo imesema “haielewi kwa nini watu wanaopinga taifa la Israel waruhusiwe kulizuru”.

Mwezi uliopita balozi wa Israeli nchini Marekani, Ron Dermer alisema wabunge hao wawili wa Democratic wataruhusiwa kuingia nchini humo “kwa heshima ya bunge la Marekani na uhusiano uliopo kati ya nchi hiyo na Israel”.

Rais Trump, ambaye ana uhusiano wa karibu na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, ametofautiana na wabunge hao kutokana na kauli tata ya kibaguzi aliyotoa dhidi yao, aliposema “warudi” katika mataifa waliyotoka familia zao.

Siku ya Alhamisi aliandika katika Twitter yake akiomba wapigwe marufuku na kuongeza kuwa”wanaichukia Israel na wayahudi wote na kwamba hakuna kitu kitakachowafanya wabadilishe msimamo wao”.

Presentational white space

Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini Marekani, viongozi hao wawili walikuwa na ziara ya kikazi Jumapili hii, ambayo pia ingelijumuisha wao kufika eneo tata la Temple Mount mjini Jerusalem, linalotambuliwa na Waislamu kama Haram al-Sharif.

Pia walikuwa na mpango wa kukutana na wanaharakati wa amani wa Israel na Palestina na kusafiri hadi ukingo wa Magharibi wa Jerusalem katika miji ya Bethlehem, Ramallah na Hebron.

Ziara ya ukingo wa Magharibi ilipangwa na shirika la Miftah, linaloongozwa na mpatanishi wa amani wa Palestina, Hanan Ashrawi.

Bi Tlaib alikuwa na mpangowa kusalia huko kwa siku mbili zaidi ili kukutana na nyanya yake katika kijiji kimoja Palestina.

Siku ya Jumatano Bw. Netanyhau alishauriana na waziri wa mambo ya ndani, Mkuu wa baraza la usalama na mwanasheria mkuu, kulingana naGazeti la Haaretz.

Israeli hufutilia mbali visa ya raia wa kigeni wanaotoa wito wa ususiaji wa aina yoyote unayolenga Israel – iwe ni wa kiuchumi, kitamaduni au kimasomo.

Sheria hiyo inajaribu kukabiliana na vugu vugu “linaususia na kuwekea vikwazo” Israel ambalo linawafuasi kadhaa Ulaya na Marekani. (chanzo BBC)