Wajasiriamali wanawake Pemba hawaisahau Corona ilivyokatisha mwendo kasi wa kipato chao

 

TAMWA iliwanyanyua kwa vifaa kinga, elimu bado wachukua tadhari  

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

DISEMBA mwaka jana, kwenye nchi China kulitangaazwa kuibuka kwa ugonjwa wa COVID- 19, ambao baadae ulisambaa kwa kasi duniani kote.

Awali waliyowengi, walidhani ugonjwa huo ni kama yale magonjwa mengine, mfano ebola ambayo huwa na kawaida ya hubakia katika nchi chache.

COVID-19 ulianza kuingia barani Afrika, ndani ya nchi ya Misri mwezi Machi mwaka huu, na kisha kusambaa kwa kasi kwenye nchi za Afrika Mashariki ikiwemo Tanzani.

Wataalamu wa afya ya mwanadamu, wanasema ugonjwa huo ni wa aina ya pekee kuwahi kutokea, kwa kule kusambaa kwake, maana kwa mfano UKIMWI ulihitaji nji kama ya kubadilishana damu au tendo la kuingiliana na mwenye virusi.

COVID 19, inasambaa kwa njia nyepesi mno, mfano mwenye ugonjwa hata chafya yake, mafua, machozi, mate achia mbali damu au kulala nae.

Ndio maana kila mmoja, hata baada ya kuingia kwa ugonjwa huo nchini Tanzania na hadi kufikia Mei 7, kuwa na wagonjwa 509, kati ya hao Zanzibar ikiripoti 134.

Tena hapo matamko ya viongozi, wakishirikiana na watalamu wa afya, yalianza kuwataka wafanyabiashara na wajasiriamali kama sio kufunga biashara zao kabisa, basi wachukue kila aina ya tahadhari.

Eneno la kisiwa cha Pemba, kama kilivyo cha Unguja, penye wajasiriamali 20, basi 12 kati yao wamewezeshwa au kuoneshwa njia na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania ‘TAMWA’ ofisi ya Zanzibar.

ATHARI ZILIZOPITA ZA CORONA KWA WAJASIRIAMALI PEMBA

Kila mmoja ni shahidi kuwa, ugonjwa wa Corona uliacha pengo kubwa kwa wafanyabiashara hata wakubwa, pale nchi ilipopiga marufuku kutoingia wala kutoka.

Biashara kama za sekta ya utalii na hata ndege za kimataifa zililazimika kusita, hivyo kuwepo kwa uhaba wa bidhaa jambo lililopelekea kuporomoka kwa uchumi.

Ndio maana Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akiwasilisha bajeti ya ofisi yake ya mwaka 2020/2021, ndani ya Baraza la Wawakilishi, alisema uchumi wa Zanzibar ulitarajiwa kukua.

Anabainisha kuwa, uchumi huo ulitarajiwa kufikia kwa asiliamia 7 hadi 8 kwa mwaka 2020, lakini uwepo wa Corona sasa unatarajiwa kukua kwa asilimia 3.

Aanasema hilo limesababishwa kutokana na kuyumba kwa sekta za uchumi ikiwemo utalii, biashara, uwekezaji na kupungua kwa mapato ya serikali.

Kama baba lao (serikali), imepata athari ya Corona, suala la kujiuliza…. je wasiriamali wetu hasa wanawake twarajia wengekuwa katika mazingira gani.

Bibi Fatma Abdi wa kikundi cha ‘Nyota njema’ cha kijiji cha Kiungoni wilaya ya Wete, anasema kabla ya Corona kwa mwaka 2019 pekee, walijipatia shilingi 1, 450,000 baada ya kuuza mikoba 45, sabuni ya maji dumu sita zenye ujazo wa lita tano tano, sabuni za miche 60 na vipochi 20 vya kisasa.

Anasema Corona kwa vile wataalamu wa afya wanataka kujiepusha na mikusanyiko, ambayo ndio waliyokuwa wakiitumia kutangaaza na kuuza bidhaa zao, mambo yalikuwa magumu.

“Unajua sisi tukisikia pahala panamikusanyiko tu  huwa tushafika na bidhaa zetu, maana ndio tulivyofahamishwa na wawezeshaji kutoka TAMWA, lakini sasa Corona ilipoingia tuliathirika mno,’’anafafanua.

Walipokosa kuzitembeza bidhaa zao kutokana na uwepo wa Corona, walikuwa na bidhaa za shilingi 279,500 ambazo zilikuwa ndani zikisubiri wateja.

Miongoni mwa bidhaa ambazo zilijiweka karantini kutokana na kuingia woga wa kuzitembeza kama zamani, ni pamoja na sabuni ya maji dumu tatu zinazojumuisha lita 15, dawa maalum ya kutolea madoa ‘Jik.

Lakini athari hii ya Corona ambayo pia kwa Tanzania imeshasababisha vifo zaidi ya watu 16 hadi Aprili 30 mwaka huu, imewakumba hata wajasiriamali wanawake mmoja mmoja, akiwemo Nassr Salum Mohamed.

Anasema katika eneo analoishi la Minungwini wilaya ya Wete, alikuwa na kawaida ya kutembeza bidhaa vile karafuu mchanganyiko kwa ajili ya kutolea nongo za mwili ‘singo’.

Kabla ya Corona, alikuwa akipita kwenye vijiji vya Mchanga mdogo, Minungwini, Kwa bikirembo, Kigongoni, Kojani, Kangangani na Ole ili kuwafuata wateja wake.

“Hakuna kijiji ambacho kwa wilaya ya Wete na Micheweni sijafika kuwafuta wateja tena kwa mguu, na huingia kila nyumba kwanza kuwasomesha na kisha kuwauzia, na narejea kwangu magharibi,’’anasema.

Anasema ujasiriamali mzuri, lazima uwe na sifa ya kuitangaaza bidhaa na kisha kuwafuata wateja walipo, ili kuwapunguzia usumbufu wa kukufuata ulipo.

Kazi hiyo za kuviandama vijiji kimoja baada ya chengine, alikwisha izoea na alikuwa akijipatia wastani wa shilingi 120,000 hadi shilingi 130,000 kwa mwezi hutegemeana na msimu.

….eee…!!!…mjasiriamali mwanamke aliyeathiriwa na Corona kiuchumi ni mimi, maana hakuwa tena na mpango wa kuwafuata wateja majumbani, ukipiga hodi waangaliwa kwa dirishani,’’anasema.

Anaeleza kuwa, tokea kuanza kwa karantini ya kuacha mikusanyiko isiyo ya lazima kwa hofu ya Corona, sasa biashara zake zilipoteza mwelekeo na kula hasara.

“Sasa mimi tokea kuanza kwa Corona kwa mwezi mapato yangu yameshuka kutoka shilingi 130,000 za kabla na nilikuwa nauza shilingi 70,000 tu,’’anasema.

Hivyo mjasiriamali huyo anasema, kama Corona yengendelea kubakia nchini, hana hakika kuwa ujasiriamali wake ambao aliwezeshwa na mradi wa uwezeshaji wa ‘WEZA II’ kuipitia TAMWA unaweza kuwa mkombozi.

Katibu wa ushirika wa ‘Tupate sote’ wa Mavungwa shehia ya Mbuzini Wilaya ya Chake Chake Meiye Hamad Juma, anasema kwao Corona imeathiri sana shughuli zao.

Kabla ya ujio wa janga hilo, walikuwa wakiiuza bidhaa zao na kujipatia wastani wa shilingi 250,000 hadi shilingi 300,000 kwa mwezi, kwa vile walikuwa na uhuru wa kuzitembeza watakavyo.

Bidhaa zao kama za mikoba ya kisasa ya ukili, inyoshonwa kwa cherehani, mafuta ya mti wa Mkaratusi, jiki na sabuni ya maji walikuwa wakiwafuta wateja hadi majumbani mwao.

“Wateja wetu ni wale wa nyumba kwa nyumba au mlango kwa mlango, ndio maana hapo ikifika mwezi tukifanya hesabu tunajikuta mpaka na shilingi 300,000 lakini sasa Corona iliwapiga karantini ya kiuchumi,’’anasema.

Athari kubwa ya Corona ndani ya kikundi hichi cha wanawake, Katibu anasema ni kushuka kwa mauzo, hadi kujipatia shilingi 75,000 na zisizozidi shilingi 80,000 kwa mwezi kwa kipindi cha corona.

Kwa hesabu za haraka haraka, utagundua kila mwezi wanawake hawa sasa walipoteza kati ya shilingi 220,000 hadi shilingi 225,000 kutokana na kukosa kutembeza bidhaa zao.

Anasema Corona yengeendelea kung’ang’ania Tanzania, safari ya kurejea kwenye umaskini, ambao walishauwaga kwa miaka zaidi ya 10 sasa, yengewadia.

Kadhia hii ya Corona pia, imebisha hodi ndani ya kikundi cha ‘Nguvu yetu ni umoja’ cha Minunwgini kinachotengeneza majani ya chai ya kileo na yenye tiba.

Kikundi hicho chenye wanachama 11 wanawake aliyojikusanya na kuamua kuukimbia umaskini, wanatengeneza mikoba ya kisasa ya ukili na pamoja na singo za karafuu.

Kupitia Mwenyekiti wake bibi Maulid Saleh Hamad, anasema walishajiandaa kwa bidhaa zenye thamani ya shilingi milioni 1, 260,000 tayari kwa safari ya mkoani Tanga, kwenye maonyesho waliyokwishaalikwa.

Wenyewe walikuwa na mikoba ya kisasa 40 kwa bei ya mmoja shilingi 30,000 inayotengenezwa kwa ukindu na kushonwa kwa cherehani na kutia kitambaa ndani, majani ya chai vikopo 100 sawa idadi kama hiyo ya vipochi.

Kikundi hichi cha ‘Nguvu yetu ni umoja’ ambacho kilianzishwa miaka tisa iliyopoita, kutokana na dunia kuingiliwa na ugonjwa huu wa Corona, mwaka 2018, waligawana faida na kila mwanachama alijipatia shilingi 60,000.

Ingawa faida hiyo ilipanda karibu mara mbili, maana mwaka 2019, waligawana kila mwanachama shilingi 110,000 baada ya kuzichana chana shilingi 1,210, 000 walizozipata kama faida kupitiza uzalishaji wa bidhaa zao.

“Unaona Corona ilivyotuvuruga, maana hata mwaka huu 2020 tunatarajia kugawa faida ndogo sana, isiyozidi shilingi 50,000 kila mmoja, maana ndio imetuendesha mchomo kwa kukosa kwenda kwenye maonyesho Tanga,’’anaeleza.

TAHADHARI WANAZOCHUKUA ZA KUJIKINGA NA CORONA

Hapa Mwenyekiti kikundi cha ‘Nguvu yetu ni umoja’ bibi Maulid Saleh Hamad, anasema ni kuendelea kuvitumia vifaa kinga walivyokabidhiwa na TAMWA

“TAMWA ilitukabidhi vifaa kama barakoa na sanitaiza, ambapo hadi sasa tunaendelea kuvitumia kama kinga ya ugonjwa wa Corona,’’alieleza.

Kumbe hata Katibu wa ushirika wa ‘Tupate sote’ wa Mavungwa shehia ya Mbuzini Wilaya ya Chake Chake Meiye Hamad Juma, anasema hadi sasa sio serikali kuu wala wizara ya Afya haijatangaaza kumalizika kwa corona.

“Kama ugonjwa haujatangaazwa kuondoka Zanzibar, basi na sisi wajariamalia tunaendelea kuchukua tahadhari kama wataalamu wa afya wanavyopendekeza,’’anasema.

Fatma Abdi wa kikundi cha Nyota njema, anasema kubwa zaidi kwa sasa ni kuwakumbusha wanakikundi wenzake juu ya kuendelea kuchukua tahadhari za kila siku.

“Vifaa walivyotupa TAMWA kama sanitaiza, barakoa na elimu ndio ambayo tunaendelea kutumia ili kuona kama ugonjwa huo upo basi hausambai,’’anasema.

TAMWA KINASEMA JE?

Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania ‘TAMWA’ ofisi ya Zanzibar, chenyewe kilikereketwa mno na uwepo wa Corona, na hasa kuona ni adui wa uchumi kwa wajasiriamali wanawake.

Mkurugenzi wa TAMWA Zanzibar dk. Mzuri Issa wakati akiwasilisha mada ya athari za Corona hasa kwa wanawake, anasema Corana ilisababisha serikali kufunga masoko kuanzia 10:00 jioni.

Anasema soko kama la wazi la Darajani mjini Unguja, kabla ya uwepo wa Corona, lilikuwa likianzia saa 11:00 jioni hadi saa 4:00 usiku, na kutoa fursa kwa wajasiriamali wengi wao wanawake kuuza bidhaa zao mbali mbali.

“Wapo wanawake, maskini na wajane wengi wanaofanya biashara kama za mazao ya chakula na biashara wakiyatumia masoko ya Mwanakwerekwe na Darajani, lakini hakufaidika  nayo kiukamilifu na kuathirika kiuchumi,’’anasema.

Kwenye eneo jengine Mratibu wa TAMWA Ofisi ya Pemba Fat-hiya Mussa Said, anasema ‘TAMWA’ iliandaa mpango wa kisasa wa kuhakikisha inawaunganisha wajasiriamali wanawake na wateja wao kwa njia ya kielektroniki.

Anasema TAMWA pia kwa wakati ule wa Corona, iliwapa elimu ya vifaa kinga wajasiriamali hasa wanawake kisiwani Pemba, ili kuona wanafanyakazi zao kwa ufanisi.

Mwisho