Waliochimba mchanga bila ya kibali wakwamisha kesi kuendelea Pemba

 

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

WATUHUMIWA watatu wanaodaiwa kuchimba mchanga eneo lisiloruhusiwa kijiji cha Tundaua wilaya ya Chakechake, hawakutokeza mahakamani, na shahidi kutoka Idara ya Misitu kujikuta akiwa peke yake, na kesi hiyo kushindwa kuendelea.

Shahidi huyo Rashid Suleiman Rashid, alitinga mahakamani hapo tayari kwa ajili ya kutoa ushahidi wake, ingawa watuhumiwa wote watatu, hawakuchomaza mahakamani hapo bila taarifa rasmi.

Shauri hilo, ambalo liko mahakama ya wilaya, kwa jana lilizimika kuhamia kwa muda na kuendeshwa mahakama ya mwanzo Chakechake, kutokana na hakimu husika wa shauri hilo, kutokuwepo nje kwa kazi nyingine.

Mara baada ya mwendesha mashitaka kutoka Jeshi la Polisi sajenti Juma Habibu, kuwaita wathumiwa hao, hakuna alieitikana na ndipo alipoamua kumuita shahidi wake mbele ya hakimu huyo.

Mara baada ya shahidi huyo kuwasili pasi na kuwepo kwa watuhumiwa, hakimu alimtaka shahidi huyo kurudi nyumbani na kufika tena mahakamani hapo, Febuari 3 mwaka 2020.

“Shahidi leo ilikuwa utoe ushahidi wako mahakamani hapa, lakini kwanza watuhumiwa hawakufika na pili hakimu husika wa shauri hili, hayupo leo mahakamani, hivyo tumeshalighairisha,’’alisema.

Hivyo hakimu huyo ameutaka upande wa mashitaka kuhakikisha watuhumiwa wanakamatwa na kufikishwa mahakamani siku hiyo, ambapo kesi yao itaendelea tena.

Awali ilidaiwa mahakamani hapo kua, watuhumiwa hao Abass Maabadi Mohamed miaka 25, Mohamed Abdalla Omar miaka 18 na Amour Ali Ampour miama 40 wakaazi wa Tundaua walidaiwa kuchimba mchanga sehemu isioruhusiwa.

Ilidaiwa kua, tukio walilolitenda siku na tarehe isiofahamika mwezi August, mwaka 2019, ambapo wakijua kuwa eneo hilo haliruhusiwi, wao walichimba mchanga huo.

Tukio walidaiwa kulifanya eneo la Tundaua wilaya ya Chakechake mkoa wa kusini Pemba, ambapo walichimba mchanga ndani ya shamba la serikali.

Ilidaiwa kua, kufanya hivyo ni kosa kinyume na kifungu cha 6B (1) sheria no 12 ya mwaka 1992, kama ilivyofanyiwa marekebisho na sheria no 15 ya mwaka 2003 na kufanyiwa mapitio mwaka 2006 sheria ya Matumizi ya Ardhi Zanzibar.

Mwisho