Wanawake: tupo tayari kugombea na tutashinda – Makombeni

mratibu wa TAMWA kisiwani Pemba Bi Fat-hiya Mussa Said akifungua mkutano wenye lengo la kuwahamasisha wanawake kushiriki kugombea nafasi za uwongozi

Imeandikwa na Salmin Juma- Pemba

Email:salminjsalmin@gmail.com

Wanawake wa shehia ya Makombeni wilaya ya Mkoani kisiwani Pemba wamesema, wapo tayari kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali  za uwongozi hasa baada ya kuona wanaume vijijni mwao wapo tayari kuwaunga mkono kwa lengo la kupata maendeleo wanayo yakusudia.

Wameyaeleza hayo jana huko kijijini kwao katika mkutano  maalum wa uhamasishaji wanawake kushiriki katika nafasi za uwongozi , mkutano ambao umeandaliwa na chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania TAMWA upande wa Zanzibar (kisiwani Pemba)

Wakizungumza kwa hasama wananchi hao  baada ya kupewa elimu na chama hicho  iliyo waonesha vipi wanawake wanaweza kuwa msaada mkubwa katika maeneo yao ikiwa watapewa nafasi  katika uwongozi, walisema  wanajiamini na wataonesha mfano wa kuigwa ifikapo 2020 katika uchaguzi mkuu.

Baadhi ya wananchi wa shehia hiyo wakimsikiliza kwa makini mtoa mada.

Kwa upande wake Mwanahija Hussein Haji alisema, awali walikua na dhana mbaya kuwa mwanamke hawezi kugombea nafasi za uongozi lakini kupitia taaluma waliyoipata wamebadilika na wataamua kuingia katika nafasi hizo.

“tunaweza sana lakini tatizo letu tuna aibu ya kuogopa kushindwa, mimi mwenyewe naweza kugombea na nina moyo huo hivi sasa” alisema mwanamke huyo.

Mwengine Asha Nassor Makame alisema “nimepata hamasa, najiamini na kuanzia leo nasema naweza kugombea uongozi, taaluma tuliyoipata leo imetuzindua sana” alisema mwananchi huyo.

Nae Bi Zuhura Faraji Kheri alisema “tushajiamini na hata wanaume washatwambia tuchukuwe uongozi”

Mkutano huo uliyowashirikisha wanawake na wanaume kijijini hapo kwa pamoja waliondoka na dhana ya kuamshana mitaani kwa lengo la kuwapa fursa wanawake hasa kwakua kuna mambo yanayowakabili akina mama na wenyewe ndio wanaoweza kuyaeleza vizuri kama vile, shuda ya maji, afya, elimu na mengineyo.

Juma Mussa Juma mwananchi kutoka shehia hiyo, alisema mbele ya hadhara kuwa “wanawake wanahuruma sana,tusiwavunje moyo kwa kusema eti watabadilika wakipata uongozi, tuendelee kuwapa hamasa, changamoto ni za kawaida” mwisho wa kunukuu.

Mwananchi mshiriki wa mkutano huo Juma Mussa akitoa mchango wake mbele ya hadhara hiyo

Alisema, kwa upande wake hana matatizo na wanawake kupewa nafasi huku akiashiria kuwa yupo tayari kumpa mashirikiano mwanamke kupata uongozi kijijini mwao.

Awali akiufungua mkutano huo, mratibu wa TAMWA kisiwani Pemba Bi Fat-hiya  Mussa Said aliwataka wanawake kuacha dhana ya kuwa kila kitu wafanyiwe na badala yake wanaweza kusimamia mambo yao kama wanawake na yakawa sawa.

Pia aliwataka akina baba kujijini hapo kuwaunga mkono wanawake katika nafasi za kugombea uongozi ili wapate kuwasilisha mambo yao na ya kijamii kwa ujumla.

Mmoja miongoni mwa wanaume mawakala wa mabadiliko (Male Change Agent) kutoka TAMWA Pemba Mr Omar Mjaka Ali akiwahutubia wanakijiji hao alisema mwanamke kua kiongozi sio jambo geni,kwani wapo wengi na wanaonekana, hivyo wasiogope kugombea nafasi hizo ili wakafikishe vilio vyao katika mamlaka husika

“hawa ni waandishi wa habari wanawake, wametoka mbali kukuleteeni elimu hii, ipokeeni kasha muchukue hatua,wanakupendi hawa”alisema Mr Omar.