Washindwa kufikishwa mahakamani Pemba kwa gari ya Polisi kukosa mafuta

sio gari hilisi hii 'kumradhi'

 

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

ZAIDI ya kesi 15 za aina mbali mbali zikiwemo za vitendo vya udhalilishaji na dawa za kulevya, zimeshindwa kuendelea kusikilizwa, kwenye mahakama za wilaya, na mkoa Chake Chake, kutokana na Jeshi la Polisi, kutowasilisha mahabusu kutoka rumande.

Taarifa kutoka kwenye mahakama hizo zinaelea kuwa, Jeshi la Polisi walishindwa kuwapeleka mahabusu hao mahakamani kutokana na ukosefu wa mafuta.

Taarifa hizo zinaeleza kuwa, tatizo hilo lilianza tokea wiki iliopita na kuendelea tena juzi Januari 27 na 28 mwaka huu, huku mahakimu wa mahakama hizo, wakilazimika kuziahirisha kesi hizo pasi na kuwepo kwa watuhumiwa.

Hakimu wa mahakama ya Mkoa ‘B’ Chake Chake Luciano Makoye Nyengo, alisema jambo hilo linaathiri kwanza utendaji na malengo yao ya kuziendesha kesi hizo.

Jengine linaloathiri ni kupoteza fedha bila ya matumizi halali wanazolipwa mashahidi kutoka miji mbali mbali ya Pemba, ambao mahakama walishawalika kufika mahakamani kutoa ushahidi.

Hakimu huyo alisema juzi Januari 27 alielezwa kuwa, gari ya mahabusu yenye kawaida ya kuwachukua watuhumiwa hao kutoka Wete ilikosa mafuta, hivyo kushindwa kuwafikisha watuhumiwa.

Alieleza kuwa, pia Januari 28, alipata taarifa kuwa gari husika ilipata hitilafu, jambo ambalo anasema lazima kuandaliwe utararibu ambao, hautapelekea mahabusu kutofikishwa mahakamani.

“Hadi leo ‘juzi’ Jumanne ya Januari 28, tuna karibu kesi 10 kwenye mahakama hii ya Mkoa ‘B’ pekee ambazo tumeshalazimika kuziahirisha kutokana na watuhumiwa kutoletwa, ukiulizwa unaambiwa gari haina mafuta au imepanguka ‘gear box,’’alieleza.

Baadhi ya mashahidi waliofika mahakamani kutoa ushahidi wao pasi na kusikilizwa, walisema hali hiyo inawawiya vigumu wao kwa mara nyingine kufika mahakamani hapo.

Mohamed Omar wa Mkoani, alisema alifika mahakamani kuanzia saa 1:58 asubuhi akisubiri kuitwa mahakamani kutoa ushahidi wake, na alijibiwa saa 4:55 kuwa watuhumiwa hawakuletwa.

“Nilidhani mapema kabla ya kesi kuanza kama mahabusu hawaletwi na sisi tuarifiwe mapema, maana tunashughuli zetu nyingine, sisi sio waajiriwa wa mahakama,’’alieleza.

Nae Khamis Omar alisema, usumbufu kama huo na ule wa aina mwengine wa kuwa hakimu au jaji husika hayupo, ndio unaowavunja moyo, baadhi ya wananchi na kuwa wagumu kuhudhuria mahakamani.

Kamanda wa Polisi mkoa wa kusini Pemba Ahmed Khamis Makarani kila anapofuatwa na mwandishi w ahabari hii kujibu tuhuma za kutofikishwa kwa mahabusu hao hakuwa akipatikana ofisni kwake.

 

Kamanda huyo alifuatwa na mwandishi wa habari hizi kuanzia Januari, 31, Febuari 3, na Feubuari 4 bila ya mafinikio, ingaw ajuhudi za kumtafuta ili aelezee juu ya kadhia hii zinaendelea.

Miongoni mwa kesi zilizolazimika kuahirishwa Januari 28 na pamoja na Ramadhan Omar Ramadhan anaekabiliwa na tuhma za kuvunja na kuingia duka na kuiba, Abass Lula Mohamed anaedaiwa kumshambuli mwenzake kwa kisu.

mwisho