Watoto Micheweni wataka wadhalilishaji waanzie miaka 50 kifungo

 

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

WATOTO katika shehia ya wilaya ya Micheweni mkoa wa kaskazini Pemba, wamevitaka vyombo husika ikiwa vina nia ya kweli ya kutokomeza matendo ya udhalilishaji kwa wanawake na watoto, kuongeza muda chini ya vifungo kwa wadhalilishaji, kutoka miaka 30 ya sasa hadi kufikia miaka 50.

Walisema adhabu ya chini iliomo kwenye sheria mpya ya Adhabu no 6 ya mwaka 2018 kwenye vifungu vya 108 na 111 ya kifungo cha miaka 30 ni kidogo, na sasa mahakama ziangalie uwezekano wa kuanzia na miaka 50 hadi kifungo cha maisha.

Wakizungumza na www.pembatoday.com, kwenye shehia hizo, walisema matendo hayo, yamekua yakiongezeka kutokana na wanaotiwa hatiani, kupewa adhabu kama vile miaka saba, 10, au 15, na sasa wakati umefika kwa adhabu hiyo, kuanzia na miaka 50 hadi kifungo cha maisha.

Mmoja kati ya watoto hao, mkaazi wa shehia ya Shumba vyamboni Saada Ilinini Mohamed, alisema iwapo kutakua na adhabu hiyo, kwa washitakiwa wawili tu, wengine wanaweza kuingia woga.

“Mimi napendekeza kama serikali inataka kuondoa matendo haya yanayotudhalilisha, basi sasa kifungo kidogo kwa atakaetiwa hatiani, kianzie miaka 50 na sio 30,’’alisema.

Alisema matendo hayo kwenye shehia yapo kwa baadhi ya waalimu wa madrassa, skuli na vijana wengine, kuwadhalilishaji wanawake na watoto.

Nae mwanafunzi wa darasa la nne skuli ya msingi ya Shumba vyamboni Mohamed Abdalla Saadi, alisema matendo hayo kwenye shehia yapo ya kutisha, kwa watoto kupelekwa vichakani.

Alisema njia moja ya kuyaondoa ni kwale wanaofikishwa mahakamani wafungwe kifungo kirefu cha kuanzia miaka 50 na kuendelea.

“Ili kuyaondoa matendo haya, kwanza kila mmoja atoe taarifa kwao au kwa sheha, lakini na atakaefikishwa mahakamani, afungwe sana,’’alipendekeza.

Kwa upande wake Hassina Omar Hamad wa Konde alisema, wakati umefika sasa kwa mahakama, kutowafumbia macho wale wanaotiwa hatiani kwa udhalilishaji.

“Rai pekee ni kuwafunga mapaka wachoke huko ‘gerezani’ chuo cha mafunzo wakae mapaka wawe wakongwe na wengine wafungwe miaka 50 au maisha,’’alipendekeza.

Watoto hao walisema, udhalilishaji uliotawala kwenye shehia zao ni pamoja na ulawiti, ubakaji na kukashifu, kazi inayofanywa na baadhi ya waalimu wa madrassa hasa wanaopigisha madufu.

Sheha wa shehia ya Shumba vyamboni Time Said Omar, alikiri kuwa, matendo ya udhalilishaji kwa sasa, yameshamiri zaidi kwenye shehia hiyo, ambapo watuhumiwa wakiwa ni baadhi ya waalimu wa madrassa.

“Ni kweli hata ndani ya shehia yangu, yupo mwalimu wa madrassa Ali Hamad Juma, anatuhumiwa kuwaharibu wanafunzi wake zaidi ya saba (7), ingawa ameshahojiwa Polisi,’’alieleza.

Alisema hatua iliochukuliwa kwa sasa kwa mwalimu huyo, kwanza ni kufukuzwa chuoni na kisha kufikishwa kituo cha Polisi Micheweni kwa kuhojiwa.

Nae Asaa Ali Ameir miaka 50, wa kijiji cha Mamoja Shumba vyamboni wilaya ya Micheweni, alisema matendo ya udhalilishaji kwenye shehia hiyo, yameibuka kwa kasi katika miaka ya hivi karibuni.

Alieleza, kama hatua zitachukuliwa kuanzia ngazi ya shehia  na kuwepo kwa ushirikiano wa dhati na kisha wilaya, mkoa na taifa, matendo hayo yanaweza kuwa ndoto.

“Ninachokiona bado kuna mkatiko, mmoja anachukua hatua dhidi ya mtuhumiwa na mwengine analegeza nguvu, sasa hapa huwa tunawapa mwanya wanaofanya matendo kuendelea,’’alieleza.

Kwa upande wake mzazi alieharibiwa mjukuu wake na mtoto wa kaka yake, shehia ya Konde, alisema matendo hayo yapo, kwa sababu wanaofanywa hawana adhabu kali.

Nae mwalimu mkuu wa skuli ya sekondari ya Konde Rashid Muhudhwari Juma, alisema watoto wanaofanyiwa matendo hayo, hawajajengwa kielimu na namna ya kumjua mdhalilishaji.

Alisema njia pekee ya kuyaondoa matendo hayo, ni kwa wazazi kuwa makini, kuanzia watoto wakiwa wachanga ili wawakinge na watu wabaya, wanaoweza kuwaingiza kwenye matendo hayo.

Nae kiongozi wa dini ya kiislam wilaya ya Micheweni sheikh Omar Khamis Hamad, alisema matendo hayo yapo sio tu kwa waalimu wa madrassa pekee, bali kila eneo kuanzia hata kwenye ofisi za umma.

“Inaumiza mara mbili unaposkia kiongozi wa dini au mwalimu wa madrassa kwamba amemuharibu mwanafunzi wake, sasa mzazi anajiuliza niwapelekee wapi watoto wangu,’’alihoji.

Sheha wa shehia ya Konde Mohamed Omar Abdalla, alisema katika miezi miwili ya mwishoni mwa mwaka jana, alipokea matukio 13 ya watoto kudhalilishwa.

Alisema miongoni mwa kesi hizo, wapo watuhumiwa wako rumande, na wengine Jeshi la Polisi likiendelea na upelelezi na wengine wakiwa wamekimbilia mkoani Tanga.

“Kati ya hao yumo mzee mmoja anaefikia miaka 100, mlezi, mwalimu wa skuli, madrassa na wengine ambao wamewadhalilishaji watoto na wengine wameshakamatwa,’’alieleza.

Mkuu wa wilaya ya Micheweni Salama Mbarouk Khatib, alisema njia nyingine ya kumaliza matendo ya udhalilishaji, ni jamii kushirikiana na vyombo husika, ikiwemo Polisi na Mahakama.

Alisema, katika kufanikisha hilo, bado marufuku ya mwisho saa 12:00 jioni upigaji wa dufu na kuonesha tv nje inaendelea.

Alisema katika utafiti wao mdogo walioufanya, waligundua kuwa, upigaji dufu kiholela, ambao watoto huwa nje ya makaazi yao kwa muda mrefu, unachangia udhalilishaji.

“Wapo watoto kadhaa baada ya kuhojiwa wanasema, wamelawitiwa kwenye madufu na kwenye vyuo vya kur-an hasa vya nyakati wa usiku, ndio maana tumepiga marufuku,’’alifafanua.

Alifahamisha kuwa, walipata maelezo ya watoto hao kwa kutumia kauli mbiu yao ya ‘pasuka vunja ukimnya’ ambapo alishafanya mikutano kwenye shehia zote juu ya kuzungumza na wazazi kuhusu matendo hayo.

Mratibu wa Chama cha waandishi wa habari Wanawake Tanzania ‘TAMWA’ Pemba Fat-hiya Mussa Said alisema, TAMWA, imekuwa ikishirikiana kwa karibu na waandishi wa habari ili kuyaibua na kisha kuyaripoti matendo hayo.

Alisema moja ya njia yakutokomeza matendo hayo, ni kwa vyombo vya habari kuyaripoti kuanzia siku ya mwanzo ya tukio hadi linapofikishwa mahakamani na kuhukumiwa.

“Kama waandishi wa habari watazidisha kasi ya kuyaibua na kisha kuyasambaaza kwa jamii, nadhani inaweza kuwatia hofu wale wanaoendesha vitendo hivi,’’alisema.

Katika hatua nyingine, alisema wamekua na mafunzo kadhaa ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari, ikiwa ni pamoja na namna ya kuyaandikia kwa kina bila ya kuwadhalilisha wahanga.

Mwisho