Waziri Aboud Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 yafungua ajira kwa wote

 

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

MAKAMU wa Pili wa rais Zanzibar Mhe: Balozi Seif Ali Iddi, amesema moja ya shabaha na azma ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, ilikuwa ni kuwapa ajira za kudumu wananchi kupitia viwandani, ambapo sasa hilo limedhihirika kwa vitendo ndani ya miaka 56, tokea kufanyika kwa mapinduzi hayo.

Alisema hata kupitia Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020, ambayo ilinadiwa na rais wa sasa wa Zanzibar Mhe: dk Ali Mohamed Shein, iliwaahidi wananchi kuwapatia ajira kupitia viwanda hapa Zanzibar.

Makamu wa Pili aliyaeleza hayo kwenye hutuba yake iliosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Nchi Afisi ya Makamu wa Pili wa rais Mohamed Aboud Mohamed, mara baada ya kuzindua mitambo mipya ya kiwanda cha mafuta na ariki ya mimea Wawi Chakechake, ikiwa ni shamra shamra za miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Balozi Seif alisema, baada ya mapinduzi ya Zanzibar, serikali chini ya Chama cha Mapinduzi CCM, ilijipanga na kuhakikisha wananachi wake, wanapata ajira za kudumu, kupitia viwanda mbali mbali.

Alisema shabaha hiyo ya Mapinduzi na utekelezaji wa Ilani, sasa imekuwa ukionekana kwa vitendo, kwa mfano kwenye kiwanda hicho kilichopo Wawi, ambacho kimetoa ajira kadhaa kwa wananchi.

Alieleza kuwa, ilishatangaazwa tokea mapema kua, sasa baada ya kujitawala wenyewe, unyonge, umaskini, unyonyaji na ukandamizaji uondoke na wananchi wafaidike na matunda ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.

“Leo tumeshazindua mitambo mipya ya kuchakatia mafuta ya makonyo na arki ya mimea, haya ndio mapinduzi na huku ndiko kuitekeleza Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 kwa vitendo,’’alisema Balozi Seif.

Katika hatua nyingine, Makamu huyo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, aliwataka wananchi wa Wawi na vitongoji vyake, kulima mazao na mime, ambayo wataweza kuyauza kiwandani hapo.

“Sasa hapa makonyo, majani ya mkaratusi, michai chai yote yananunuliwa na mali ghafi nyingine, hii ni fursa kwa wananchi na hasa vijana, ambao wanalilia ukosefu wa ajira,’’alifafanua.

Aidha aliutaka uongozi wa kiwanda hicho, kuendelea kuwapa mafunzo ya kisasa watendaji wao, ili kumudu utendaji wa kazi kwa mujibu wa vifaa vya kisasa, vilivyofungwa ndani ya kiwanda hicho.

Alieleza kua, likifanyika hilo kiwanda hicho kitaendelea kuwa chachu kubwa ya kuongeza pato la taifa, kwa vile mafuta yanayozalishwa hapo kwa asilimia 80, huuzwa hata nje ya nchi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Taifa la Biashara la Taifa Zanzibar ‘ZSTC’ Zanzibar dk Seif Said Mzee, alisema kiwanda hicho, katika miaka ya hivi karibuni, kilikuwa kikikabiliwa na uchakavu wa mitambo yake.

Alisema, kutokana na kuchoka kwa mitambo hiyo, ndio maana ilikuwa ikiligharimu shirika fedha nyingi, kwa kule kuyafanyiwa matengenezo kila wakati.

“Kwa vile kiwanda hichi kinaiingizia mapato serikali kuu, ndio maana mwaka 2017, ZSTC liliamua kutafuta ufumbuzi wa muda mrefu, wa kuwa na mitambo mipya ya uzalishaji, ili kuondokana na tatizo la kutengeneza kila siku,’’alieleza.

Mkurugenzi huyo Mwendeshaji, alisema kampuni ‘Kunsham Asia Aroma’ ya China, ambayo awali ilikuwa ndio wateja wao, walikubali kukifanyia matengenezo kiwanda hicho, baada ya kufika kisiwani Pemba mwaka 2017 kukitembelea.

“Ziara ya kampuni hiyo, ilizaa matunda maana baadae walitiliana saini makubaliano ya awali na ZSTC na kisha kufungwa boila mpya na vyungu vitano vipya, kwa ajili ya kuzalishia mafuta ya mimea, kiwandani hapo,’’alifafanua.

Kuhusu majukumu ya ZSTC kwenye mradi huo, alisema ni kuongeza mashamba ya upandaji mikaratusi, na tayari hilo wameshafanikiwa, kupewa eneo lenye ukubwa wa ekari 256 wilaya ya Micheweni.

Nae Wziri wa Biashara na Viwanda Mhe: Amina Salum Ali aliipongeza serikali kwa kuendelea kukilea kiwanda hicho, hadi kufikia leo, kupata mitambo mipya, ambayo yataongeza kasi ya uzalishaji mafuta.

Alisema pamoja na kuongeza kasi, pia kitakuwa chachu ya kuzalisha ajira mpya kwa wananchi wa Unguja na Pemba, kwa kule kuanzisha kilimo ambapo mazo yao, wataweza kuyauza kiwandani hapo.

“Fursa ya kupanda mikaratusi, michachai na hata mikarafuu, muda ndio huu, maana tumeshaelezwa kuwa, kiwanda hichi kinahitaji malighafi kwa wingi, ‘alieleza.

Katika hatua nyingine, Waziri huyo wa Biashara, alisema kama kuna watu hawajaona faida ya Mapinduzi, wanahitajika kufunguliwa macho kwa kuoneshwa kiwanda hicho.

Kiwanda cha mafuta ya makonyo na arki ya mimea Wawi wilaya ya Chakechake, kimeanzishwa miaka 37 iliopita, ambapo baada kufungwa mitambo mipya na kampuni ya Kunsham Asia Aroma ya China, sasa kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 200 za mafuta aina ya Mkaratusi kwa mwaka.

Ambapo kampuni hiyo, kabla ya kufungwa kwa mitambo hiyo Disemba 2018, ndio iliokuwa mteja mkubwa wa mafuta yanayozalishwa kiwandani hapo, ambapo baada ya mitambo kuwa michakavu, ilivutika kufungwa mitambo mipya.

Awali mitambo iliokuwepo, ilikuwa ikipoteza wastani wa kilo  60 za mafuta ya makonyo, yenye thamani ya shilingi milioni 2.1 ambayo yalikuwa yakipotea kila saa moja ya uzalishaji.

Mradi huo umegharimu wastani shilingi bilioni 5.520 ambao ni mkopo wa masharti nafuu, unaotakiwa kurejeshwa katika kipindi cha miaka sita ijayo.

Mwisho