Waziri Hamad: Ataja faida za kunawa mikono kila wakati

 

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

WAZIRI wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Mohamed amesema, mikono isiyo safi ni chanzo kikuu cha kuchukua maradhi na kuyatia mwilini hivyo, ameitaka jamii kulichukulia jambo la kuosha mikono kuwa ni la kawaida kwa kila mmoja.

Alisema, uwepo wa maradhi ya COVID19 unalazimisha a haja ya kuzidisha bidii iliyopo sasa ya usafi wa mikono na kuwa pamoja kati ya tamaduni zetu kwani matumizi ya maji yametajwa na kuhimizwa hata katika vitabu vya dini.

Aliyasema hayo alipokua akizungumza katika maadhimisho ya siku ya unawaji mikono Duniani yaliyofanyika katika ukumbi wa Samail Gombani Chake chake Kisiwani Pemba.

Alieleza, Wizara inawajibu wa kutilia mkazo suala la unawaji wa mikono pamoja na jamii, kwani takwimu ya Dunia inaonesha kati ya nchi 60 zenye maambukizo ya juu ya CORONA kila watu wawili kati ya watatu wamekosa huduma za usafi wa mikono majumbani ikiwemo maji ya kutiririka na sabuni.

Sambamba na hilo alisema, maeneo ya skuli, vituo vya afya, hospitali na sehemu nyengine za wazi pia zinakosa nyenzo na vifaa vya usafi wa mikono hali ambayo inapelekea watoto, walimu, wagonjwa na matabibu kuwa katika hatari kubwa ya kupata maambukizi.

“Tunahitaji kuhakikisha tunakua na mpango endelevu wa ufikishaji wa taaluma katika sehemu zote za nchi juu ya umuhimu wa usafi wa mikono na mazingira,  mpamgo huu unahitaji nguvu ya pamoja ya ufuatiliaji na utekelezaji kwa wadau wote” alisema.

Alisema, katika kuadhimisha siku hiyo, wizara kwa kushirikiana na wadau, wanakua na harakati za kuishajiisha jamii juu ya umuhimu wa usafi wa mikono kwa lengo la kujikinga na maradhi kama vile Kipindupindu, minyoo, kikope cha macho, macho tongo na maradhi ya mfumo wa kupumua ikiwemo COVID19.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Kinga na Elimu kutoka Wizara ya Afya Zanzibar Fadhil Mohamed Abdalla alisema, siku hiyo ni muhimu kwa jamii hivyo aliwataka wananchi kuchukua jitihada ya kuelimishana zaidi juu ya suala la unawaji wa mikono.

“Maadhimisho haya yawe ni kama kielelezo cha kuhamasishana katika jamii zetu katika suala zima la unawaji mikono kwani jambo hili ni asilimia 40 katika kujikinga na lazima tulipe kipaumbele,” alisema.

Alisema Serikali na Wizara kwa ujumla iliamua kwa makusudi kufanya maadhimisho hayo katika kisiwa cha Pemba ili kwenda sambamba na Dunia nzima kudumisha tabia ya jamii kunawa mikono.

Nae Mkurugenzi Kitengo cha Elimu ya Afya Zanzibar Halima Ali Khamis alisema, miongoni mwa maradhi 10 yanayochukua nafasi ya juu yanayosumbua wananchi wa Zanzibar ni maradhi yanayochangiwa kwa kutokunawa mikono.

“Maradhi haya yanajumuisha homa ya mapafu, mafua ya kawaida na kuharisha na watu waliowengi wao wanaishi katika sehemu za misongamano na maeneo ambayo hayaridhishi” alisema.

Hata hivyo alisema, kupitia siku hivyo Wizara imefanya kazi kubwa ya kuelimisha jamii ikiwemo utoaji wa taaluma katika taasisi mbali mbali, mafunzo ya vitendo na vipindi katika Televisheni, Redio.

Wizara ya Afya kwa kushirikiana na wadau mbali mbali wa maendeleo Zanzibar huungana pamoja na nchi nyengine duniani kote katika kuadhimisha siku ya kuosha mikono kila ifikapo Oktoba 15 ya kila mwaka.

Maadhimisho ya unawaji mikono duniani yalianza tokea Augost, mwaka 2008 katika wiki ya maji duniani nchini Sweeden ambapo ujumbe wa mwaka huu ‘osha mikono okoa maisha’.

                                           MWISHO.