Waziri Mbarawa: PBZ inatakeleza kwa vitendo azma ya Mapinduzi ya 1964

 

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

WAZIRI wa Maji na Umwagiliaji wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Prf: Makame Mnyaa Mbarawa, amesema azma ya mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 ya kuwainua wananchi kiuchumi, yanatekelezwa kwa vitendo na Benki ya watu wa Zanzibar PBZ.

Alisema benki hiyo pamoja na nyingine duniani kote zilikumbwa na changamoto ya za kiuchumi, hali iliopelekea matawi kadhaa ya PBZ kuweza kufungwa, ingawa baade yalijifufua na kuchangia pato la taifa la shilingi bilioni 8.9 kwa mwaka 2018 na kukuza miradi ya maendeleo.

Waziri Mbarawa alieleza hayo mara baada ya ufunguzi wa matawi pacha ya PBZ kwenye hafla ya moja ya matawi hayo mjini Wete Pemba, ikiwa ni shamra shamra za miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.

Alisema, mapinduzi ya Zanzibar, yalilenga kuwakomboa wazanzibari na unyonge wa kipato, waliokuwa nao wakati wakitawaliwa, na sasa ndani ya miaka 56, Benki ya Watu wa Zanzibar ‘PBZ’ imekuwa ikiongoza katika mapambano hayo.

Alieleza kuwa, ni jambo jema kwa kipindi kilichopita kwa viongozi wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kukataa kuibinafsisha benki hiyo, ambayo leo imekuwa ikiwasaidia wananchi kuondokana na umaskini kwa kutoa mikopo mbali mbali.

“Kama viongozi wetu wengekuwa na mauono mdogo wakati uchumi wa benki ulipotetereka na kuamua kuibinafsisha, leo tusingekuwa na chakujivunia, lakini sasa twashukuru yale malengo ya mapinduzi ya kuwaondolea wananchi hali ya ngumu ya maisha, sasa yanafanywa na PBZ kwa vitendo,’’alieleza Waziri Mbarawa.

Katika hatua nyinge, waziri huyo alisema, PBZ imekuwa mstari wa mbele katika kulipa kodi serikali, jambo ambalo anaamini linatokana na utendaji wa kazi kuanzia bodi, uongozi na watendaji wake wote.

Alifahamisha kuwa, miongoni mwa wadau wakuu wanaopiga vita umaskini nchini hasa baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ni PBZ, kwa kule fedha za kodi wanazolipa kuingia moja kwa moja kwa wananchi, kwa njia ya miradi mbali mbali kama vile barabara na huduma ya maji safi na salama.

“Pamoja na hilo,  zinapojengwa barabara huzaliwa ajira za muda kwa wananchi, lakini pia ujenzi wa barabara huwapunguzia gharama za usafirishaji uwe wa mazao au bidhaa na hata wananchi wenyewe,’’alifafanua.

Alifafanua lengo la Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 la kuwamilikisha wazawa nguvu za kiuchumi, linaonesha kufanikiwa wazi wazi na kufanyika kwa vitendo kupitia PBZ.

Hata hivyo, ameutaka uongozi wa PBZ, kuhakikisha wanaongeza idadi ya wateja wake katika tawi hilo jipya la benki lililopo Wete mjini, ili amza ya kulifanyia matengenezo jengo lililokuwa la hoteli na sasa kuwa tawi la PBZ lifanikiwe.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa PBZ Zanzibar Juma Ameir Hafidh, alisema walilazimika kufanya mpango wa kuwa na tawi hilo, ambalo zamani lilikuwa hoteli ya serikali, ili kuwatimizia kiu wateja wao waliotaka tawi katika mji wa Wete.

Alieleza kuwa, ndio maana kuanzia mwaka 2016 serikali iliwapa PBZ jengo hilo, kwa ajili ya kulifanyia matengenezo na mwaka 2018 walilifanyia matengenezo hadi kufikia kuhamia.

Alieleza kuwa, ndipo alipopatikana mjenzi ya kulifanyia matengenezo makubwa na kutumia shilingi bilioni 1.7, na mapema mwishoni mwaka 2019, kazi hiyo ilikamilika.

Nae Katibu Mkuu wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar, Khamis Mussa Omar, alisema benki hiyo ndio kongwe hapa nchini na sasa imeshapata mafanikio makubwa, kwa serikalini na hata wateja wenyewe.

Alieleza kua, mafanikio mengine ya benki hiyo kuanzia mwaka 1989, ilikuwa na matawi 10 Unguja manne na Pemba matawi sita ya kutoa huduma kwa wananchi wa Kengeja, Konde, Mkoani, Micheweni, Wete na Chakechake.

“Ingawa baadae kutokana na mtikisiko wa kiuchumi, matawi ya PBZ yalipunguzwa kutoka 10 hadi matatu, sambamba na kupunguza idadi ya wafanyakazi kutoka 232 hadi 70 katika mwaka 2006,’’alifafanua.

Hata hivyo Katibu Mkuu huyo, alisema kwa sasa PBZ inaomtaji wa kutosha kama inavyotakiwa na msimamizi wa huduma za benki nchini, ambapo ni Benki kuu ya Tanzania ‘BoT’.

“Sasa PBZ iko vizuri, kwa mfano 2018 ilipata faida ya zaidi ya shilingi bilioni 24.7, ililipa kodi ya mapato zaidi ya shilingi bilioni 8, na kisha kutoa gawiyo serikali shilingi bilioni 3.4, na sisi tunaongoza kwa mashirika yote ya serikali,’’alieleza.

Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa, alisema PBZ imekuwa ikitekeleza Ilani ya uchaguzi kwa vitendo kwa kule kuwasogezea wananchi huduma hiyo.

Hata hivyo Mkuu wa mkoa wa kaskazini Pemba, Omar Khamis Othman, alisema ufunguzi wa tawi hilo jipya la PBZ litawapunguzia gharama wananchi wa Wete kwenda Chakechake.

Alisema sasa watapata huduma zote kamili, ikiwemo huduma za kifedha kwa benki ya kiislamu, jambo ambalo hapo awali walilazimika kwenda tawi la PBZ Chakechake.

Matengenezo makubwa na baadhi ya maeneo kujengwa upya, kwenye jengo la awali na hoteli ya serikali, na sasa kuwa tawi kamili la PBZ, kazi hiyo imegharimu wastani wa shilingi bilioni 1.3, kazi ilioanza mwaka 2018 na kumalizika mwishoni mwa mwaka jana.

Benki ya watu wa Zanzibar PBZ ambayo ilianzishwa Juni, 30 mwaka 1966, ilikuwa na matawi mawili pekee, ambapo hadi sasa kufikia 14, kuwa na mashine za kutolea pesa 31 na mawakala kadhaa jambo ambalo kabla halikuwepo.

Mwisho