ZAC: ”Wanaume nendeni pamoja na wenza wenu kliniki”

 

IMEANDIKWA NA ZUHURA JUMA, PEMBA

WAUGUZI wakunga wametakiwa kuacha tabia ya kuwazuilia huduma akinamama wanaokwenda kujifungua kwa kisingizio cha kwamba baba hakuhudhuria klinik, ili kuepusha matatizo yanayoweza kujitokeza.

Akijibu maswali ya waandishi wa habari katika kikao cha kutathmini kazi walizofanya kupitia mradi wa Afya kamilifu (AMREF), Mwanasheria kutoka Tume ya UKIMWI Zanzibar Saada Mussa Said alisema, kuna baadhi ya akinamama wanaokwenda kujifungua huzuiwa kupata huduma kwa sharti la mtu mwengine.

Alisema kuwa, wauguzi wakunga hawapaswi kumzuilia huduma mama anaekwenda kujifungua kwa sababu tu baba hakuhudhuria kliniki, kwani wanaweza kupoteza maisha yake na mtoto.

“Kwa kweli huwezi kumzuiza mama huduma wakati ameshakuwa tayari kujifungua, wanahatarisha maisha yake, kwani kuna baadhi ya akna baba hawataki kabisa kuhudhuria kliniki”, alisema.

Aliwataka akina baba kuhudhuria kliniki ipasavyo, ili kuondosha migogoro inayoweza kujitokeza wakati mama anapohitaji huduma katika vituo vya afya.

Kwa upande wake Ali Mbarouk Omar kutoka ZAC Pemba alisema, pamoja na kuwa ni muhimu kwa akina baba kuhudhuria kliniki, lakini haipaswi kwa wauguzi wakunga kuwazuilia huduma akinamama wakati wanapokwenda kujifungua.

“Mama anapokwenda kujifungua apewe huduma kwa vile yeye alikuwa anahudhuria kliniki kama kawaida, sio kuzuia magamba yao, isipokuwa wauguzi wakunga wafuate taratibu za kujikinga”, alieleza.

Akiwasilisha mada ya unyanyapaa Sihaba Saadat kutoka ZAC Zanzibar alisema, uelewa mdogo kwa wananchi juu ya VVU na AIDs unasababisha kuongezeka kwa unyanyapaa katika jamii.

“Unyanyapaa unaathiri kila sehemu kwani wengine hukoseshwa fursa muhimu, hivyo ipo haja ya kuelimishwa jamii ili kupunguza unyanyapaa”, alisema.

Alisema kuwa, ipo haja ya kushirikiana zaidi ili kuisaidia jamii kupambana na virusi vya Ukimwi na UKIMWI.

Kwa upande wao waandishi wa habari walilalamikia baadhi ya watendaji kuwakosesha taarifa muhimu, jambo ambalo linawapa wakati mgumu wanapotaka kuandika habari za UKIMWI.

“Kwa kweli tunahangaika sana tunapotaka kufanya habari hizi, jambo ambalo linatufanya taache kuandika habari za kuelimisha jamii kuhusu UKIMWI”, walisema waandishi hao.

 

Waliomba kuwepo na ushirikiano wa hali ya juu kama taasisi nyengine zilivyo, ili kuendelea kuielimisha jamii, jambo ambalo litasaidia kupunguza maambukizi mapya ya VVU.

Kikao hicho cha kutathmini kazi za waandishi wa habari, kimeandaliwa na Tume ya Ukimwi Zanzibar chini ya mradi wa Afya Kamilifu (AMREF).

MWISHO.