‘ZNBC tunashirkiana na ZNCC kuwasafisha njia wafanyabiashara Zanzibar’

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

BARAZA la Taifa la Biashara Zanzibar ‘ZNBC’ limesema linafanya kazi kwa karibu mno, na Jumuiya ya Wafanyabiashara Zanzibar ‘ZNCC’ kwa lengo la kuziainisha na kuziondoa changamoto za wafanyabiashara, ikiwemo ni pamoja na suala la wakusanyaji wa ushuru na mapato kwa njia za kielektroniki.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mtendaji wa baraza hilo Zanzibar Bakar Haji Bakar, wakati alipokuwa akijibu hoja za wafanyabiashara na wanachama wa ‘ZNCC’ kwenye mafunzo ya kuwajengea uelewa, juu ya kufanya utetezi kwa sekta binafsi, mafunzo yaliofanyika mjini Chakechake.

Alisema, inawezekana sana, wapo wafanyabiashara na wajasiriamali wingine, wanataka hasa kulipa kodi, utoaji wa ushuru na matozo mingine mbali mbali, lakini shida wanayokumbana nayo, ni kutokuwepo kwa kituo kimoja cha ulipaji wa kodi hizo.

Alisema, ndio maana ‘ZNBC’ na ‘ZNCC’ wamekuwa wakifanya kazi kwa pamoja kila siku, ili kuhakikisha changamoto kama hizo na nyingine zinazofanana na hizo, zinaondolewa hatua kwa hatua hapa Zanzibar.

Katibu Mtendaji huyo, alieleza kuwa, hilo linaweza kufanikiwa mara moja, iwapo wafanyabiashara hao na wajasiriamali wengine, watajiunga kweye taasisi za pamoja kama vile ZNCC.

“Sasa changamoto zenu kwa pamoja wala haziwezi kuondoka, iwapo jumuiya kama ya ‘ZNCC’ wapo wafanyabiashara bado hadi leo, wanafikiria mara mbili kujiunga, maana serikali kutatua changamoto ya mfanyabiashara mmoja mmoja ni vigumu, lakini mkijiunga pamoja, ni rahisi,’’alieleza.

Katika hatua nyingine, Katibu Mtendaji huyo wa Baraza la Taifa la Biashara Zanzibar ‘ZNBC’ aliitaka Jumuiya hiyo ya wafanyabishara Zanzibar ‘ZNCC’ kuyaangalia upya mabaraza ya biashara ya mikoa, kutokana na muundo wake, kutoonekana kuzingatia shida za wafanyabiashara wote.

“Niliwahi kuyatembelea baadhi ya mabaraza ya wafanyabiashara, lakini hayaonekani kuwa na umakini wa hali ya juu, na wengi wa wajumbe hasa kutoka sekta binfasi, wapo kama wao na sio kuwawakilisha wafanyabiashara wengine,’’alifafanua.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Zanzibar ‘ZNCC’ Hamad Hamad, alisema njia pekee ya kuyapunguza malalamiko na madai ya wafanyabiashara, ni kujiunga na jumuiya hiyo.

Alisema, haiwezakani hata siku, wafanyabiashara wanaotafuta mazingira rafiki ya kazi zao, lakini kila mmoja anafikisha malalamiko na madai yake, kwa wakati tu anapopata nafasi serikalini.

“Sisi ZNCC’ tumekuwa tukikutana moja kwa moja na Mwenyekiti wa ‘ZNBC’ ambae ni Rais wa Zanzibar, sasa kama wafanyabiashara tutakuwa tunakutana na kutoa changamoto zetu, ni rahisi kusikilizwa, maana serikali yetu ni sikivu,’’alieleza.

Alisema uwepo kwa Mwenyekiti wa Baraza hilo kuwa ni rais wa Zanzibar, imekuwa ni faraja kwa kule kuzitatu moja kwa moja baadhi ya changamoto zinazokuwa zinajitokeza kwenye mkutano mkuu wa baraza hilo.

Kwa upande wake Mdhamini wa ‘ZNCC’ Pemba Khalfan Amour Mohamed, alisema hakuna namna kwa wafanyabiashara wanaosaka maendeleo, kwanza ni kujikusanya pamoja.

“Njooni ofisi mchukue fomu kwa wale ambao hamjajiunga, maana hizo changamoto zenu zitakwamuka kwa sisi kuunganisha nguvu zetu kwa pamoja, na sio mfanyabiashara mmoja mmoja,’’alifafanua.

Akiwasilisha mada ya utetezi kwa sekta binafsi, mtaalamu elekezi kutoka Chuo Kikuu cha Dar-es Salaam Khalid Swabiri, alisema sifa moja ya kufanya utetezi ni kuhakikisha mfanyabiashara anatambulika rasmi.

Aidha alisema changamoto zinazowakabili wafanyabishara wa Zanzibar ni pamoja na utitiri wa kodi, jambo ambalo linaonekana kuwarejesha nyuma wao katika sekta ya uwekezaji na viwanda.

Alisema kwa mfano walioamua kuekeza kwenye sekta ya utalii wamekuwa wakilalamikia ukataji wa vibali kwa kila aina ya shughuli wanayoifanya, mfano ukumbi wa mikutano, uzamiaji pamoja na umilikiwa wa gari za kutembeza wageni.

“Unaweza kumkuta mfanyabiashara mafano wa hoteli ana vibali vitano, au anaesafirisha mazao kutoka kisiwani kimoja na chingine ana vibali au anatoa ushuru kwa taasisi zaidi ya tatu na zote ni za serikali, sasa hapa ndio kazi inapoanza,’’alifafanua.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo, walikiri kuwa utitiri wa kodi umekuwa ukiwarejesha nyuma katika biashara zao, ambapo hata upatikanaji wa faida wenyewe huwa hauridhishi.

Abubakar Mohamed Ali kutoka Jumuiya ya wazalishaji karafuu Zanzibar ‘ZAPCO’, alisema inawezekana wafanyabiashara hawakerwi na utoaji wa ushuru, ila changamoto ni kuwepo wakusanyaji wengi.

Nae Ali Mohamed Shela kutoka ‘PESTA’ alisema hata suala la sera na sheria zinazoongoza ukusanyaji wa kodi na ushuru mwingine kwa wafanayabiashara hapa Zanzibar, bado haziko rafiki, jambo linaloamsha mivutano na wakusanyaji.

Nae mjasiriamali Safia Mohamed Nzirai , alisema bado changamoto ya ulipaji kodi, inakuwa ni kikwazo kwa wafanayabiashara wadogo.

Mafunzo hayo ya siku moja yaliokuwa na lengo la kujenga uelewa kwa wanafanyabiashara, pamoja na wanachama wa Jumuiaya ya wafanyabiashara Zanzibar ‘ZNCC’ juu ya ajenda ya ya utetezi kwa sekta binafsi, pamoja na sheria ya baraza la taifa la biashara Zanzibar, yameandaliwa na ‘ZNCC’ na ufadhili wa shirika la ‘Trade Mark East African’.

Mwisho