ZRB yakabidhi msaada wa chakula kwa wanaoishi mazingira magumu Pemba

 

Kabla ya kuisoma habari hii, jua unachopaswa kujua

IMEANDIKWA NA MWANDISHI MAALUM, PEMBA

MKUU wa Mkoa wa kusini Pemba, Hemed Suleiman Abdalla, amewataka wafanyabiashara na wananchi kujenga utamaduni wa kulipa kodi zao kwa hiari, kwani mapato hayo ndio yanayowarejea wenyewe kwa mfumo wa maendeleo katika sekta mbali mbali.

Alisema nchi yoyote, haiwezi kusonga mbele bila ya kutegemea mapato kutoka kwa wafanyabiashara na vianzio vyengine, hivyo kulipia kulipa kodia na mapato mengine kwa hiari, ni moja ya nyenzo inayoiwezesha nchi kufanya shuhuli zake za kuwaletea maendeleo wananchi wake.

Kauli hiyo ameitoa ofisini kwake mjini Chake Chake kisiwani Pemba, mara baada ya kupokea msaada wa chakula kwa ajili ya wananchi wa mkoa huo, wanaoishi katika mazingira magumu, uliyotolewa na Bodi ya Mapato Zanzibar ‘ZRB.

Alisema, bado ipo haja ya lazima kwa wafanyabishara mbali mbali kuona wanalipa kodi zao kwa haraka kwenye ZRB kwani kisha huwapa nafasi watendaji kuziingiza serikali na kutekelezewa ahadi tofauti.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa wa kusini Pemba, aliupongeza uongozi wa ZRB, kwa kuupatia Mkoa wake msaada huo, katika kipindi hichi cha sikukuu, kwani wameutowa wakati maufaka.

Alisema wapo wananchi wamekuwa na hali mbaya zaidi, na wamekuwa hawana uhakika wa kupata chakula cha uhakika, lakini kufuatia msaada huo, unaweze kufurahisha nafsi zao sawa na wale ambao wanauwezo mkubwa.

Alieleza kuwa Bodi hiyo imekuwa ikisimamia majukumu yake ipasavyo chini ya usimamizi wa Kamishna wake, Joseph Abdalla Meza, kwa Unguja na kwa Pemba Mkurugenzi Marijan, hivyo Mkoa unaahidi kuendelea kushirikiana nao kwa lengo la kupiga hatuwa katika ukusanyaji wa mapato.

Wakati huo huo ZRB ilitoa msaada kama huo kwa uongozi wa mkoa wa kaskazini Pemba, ambapo mkuu wa mkoa huo, Omar Khamis Othman,aliipongeza Bodi ya mapato Zanzibar (ZRB) kwa kuona umuhimu wa kutowa msaada huo.

Alisema msaada huo utawafikia walengwa waliokusudiwa na hautokwenda pengine popote, kwani waliokusudiwa wanauhitaji kwa madhumuni ya chakula cha siku hiyo.

“ Tunauhakikishia uongozi wa ZRB, kuwa tutaendelea kushirikiana nanyi kwa hali yoyote ile ili kuhakikisha kila mwenye jukumu la kulipa mapato anatekeleza wajibu wake ipasavyo kwani misaada hii inatokana na makusanyo yao,”alieleza.

Mapema akikabidhi msaada huo kwa niaba ya mkurugenzi wa Bodi hiyo, Meneja Utawala wa ZRB Pemba Jamal Hassan Jamal, alisema kwamba bodi hiyo imeamuwa kutowa msaada huo kwa walengwa hao, ili waweze kuelewa kuwa michango wanayoitowa kwa ajili ya kulipa mapato, baadae inawarejea wenyewe kwa namna kama hiyo .

Aliwataka wananchi kuongeza juhudi ya kulipa mapato ya Serikali, kupitia shughuli mbali mbali wanazofanya ili mapato hayo yaweze kutumika kwa ajili ya maendeleo yao na taifa kwa ujumla.

“Ni wambie ananchi maendeleo munayopata yanatokana na michango yenu ya kodi, hivyo munapolipa mapato musione kama munaonewa ni wajibu wa kila mwananchi,”alisema.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mkoani Pemba, Issa Juma Ali, alisema alifurahi kuona taasisi hiyo imewapatia misaada watu wenye mazingira magumu, ili nao waweze kufurahika na familia zao.

Aliuhakikishia uongozi wa ZRB, kuwa msaada huo utawafikia walengwa kwa wakati ili nao waweze kujitayarisha na sikukuu baada ya mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Msaada wa vyakula mbali mbali ukiwemo mchele, sukari na Unga wangano wenye thamani ya million 6 kwa mikoa miwili ya Pemba, ulikabidhiwa kwa viongozi wa Serikali ya mikoa hiyo sambamba na barakoa za kujikinga na Corona.

MWISHO.