ZRB yapiga jeki ujenzi ofisi ya watu wenye ulemavu Pemba

 

IMEANDIKWA NA ZUHURA JUMA, PEMBA

BODI ya Mapato Zanzibar ‘ZRB’ imesaidia vifaa vya ujenzi na fedha taslim, kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa jengo la ofisi ya watu wenye ulemavu Wilaya ya Micheweni Pemba.

Akikabidhi vifaa hivyo vyenye thamani ya shilingi milioni 10, Kamishna wa Bodi hiyo Zanzibar Joseph Abdalla Meza alisema, wamesaidia vifaa hivyo, ili visaidie kumalizika kwa wakati ofisi hiyo.

Alisema, ni vyema wakasimamia ujenzi huo, ambao utafikia hatua ya kuezeka, ili litakapokamilika liweze kutumika katika shughuli zao mbali mbali za kujiletea maendeleo.

“Tunashukuru sana amani na mshikamano katika nchi yetu ndio uliosaidia kukusanya kodi na kuweza kuzirudisha kwa wananchi, hivyo tusimamie ujenzi huu ili uende vizuri”, alieleza Kamishna huyo.

Nae Meneja wa Huduma Nyenginezo kutoka ‘ZRB’ Pemba Abeid Omar Salim, aliwataka wananchi wajue kwamba kile kinachokusanywa na bodi hiyo,  kinarudi kwao kwani Serikali inafanya maendeleo makubwa katika jamii.

“Tunaona dhahiri kuwa Serikali inajenga barabara, inafikisha huduma ya maji safi na salama, huduma ya umeme na mambo mengine, hizo ndio faida ya mapato tunayoyakusanya”, alisema.

Akisoma risala ya ujenzi wa jengo hilo Muhammad Bakar Othman alisema, baada ya kilio cha muda mrefu kutaka ofisi yao, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Micheweni iliwapatia eneo halali la kiwanja chenye namba 209 mwaka 2009, ingawa awali walishindwa kujenga kutokana na kukosa fedha.

“Tunashukuru tulijenga hadi kozi ya nne  na kwa sasa tumepata msaada huu na tutafikia hadi hatua ya kuezeka, hivyo tunawaomba wafadhili wengine nao wajitokeze kutusaidia ili tufanye shughuli zetu za kimaendeleo”, alisema.

Nae mratibu wa Jumuiya ya watu wenye ulemavu Pemba Nassor Suleiman Nassor, akitoa shukurani kwa niaba ya Jumuiya, aliishukuru ZRB kwa kile walichokitoa na kuwataka kuzidi kuwasaidia pamoja na kuwatafutia wafadhili wengine.

“Tunashukuru sana na tumefurahi kwa msaada huu, tumepiga hatua kubwa sana, hivyo tunaomba mutusaidie tena na mututafutie wafadhili, ili tuweze kumaliza ofisi yetu”, alisema.

Kwa upande wake mwakilishi wa Jimbo la Micheweni Shaame Shamata Khamis, alielezea kufurahishwa kwake na kupata nguvu ya ziada katika kukamilisha jengo hilo, kwani anaamini litakapomalizika, litasaidia kuratibu shughuli zao ambazo zitasadia kuwaimarisha.

Alisema, atahakikisha anasimamia ujenzi huo, ili kumalizika na kuahidi kuchangia vifaa vyenye thamani ya shilingi milioni moja.

Nae mratibu wa Jumuiya ya watu wenye ulemavu Wilaya ya Micheweni Juma Kombo Hija ‘sibure’ alisema kuwa, litakapomalizika jengo hilo, wanaamini kuwa watu wenye ulemavu wataimarika kiuchumi, kwani milango miwili ya maduka, ambayo watajiendeleza katika shughul zao kiuchumi.

Katika makabidhiano hayo ya vifaa vya ujenzi, Kamishna wa ZRB alichangisha fedha kwa ajili ya hatua ya kuezeka, na zilipatikana zaidi ya shilingi milioni nane, ambapo shilingi 81,000 zilitolewa papo hapo.

Wakati huo huo, taarifa za kwenye mitandao zinaeleza kuwa, bodi hiyo  imefungua milango yake kwa mara ya pili, safari hii hadi Machi 31, mwaka huu, kwa wafanya biashara na walipa kodi wengine, kwenda kuomba msamahama wa madeni yao ya kodi, yanayotokana na adhabu, riba na faini.

Awali ZRB kwa mara ya kwanza tokea kuanzishwa kwake miaka 21 iliopita, ilianza msamaha wa kodi mwezi Juni hadi Disemba 31 mwaka 2019, ingawa baada ya kupokea maombi mengi ya msahama, sasa imeongezea tena hadi Machi 31 mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa wizara ya Fedha na Mipango Pemba hivi karibuni, Afisa Uhusiano wa ZRB Makamed Khamis Makame, alisema waliona ni vyema kuongeza muda, ili kutoa fursa kwa walipa kodi, kusawazisha madeni yao ya kodi.

Alisema, iwapo mlipa kodi atajitokeza katika kipindu hichi kuomba msamaha wa kodi ‘tax amnesty’ ataangalia kodi yake ya kawaida na hatoingizwa kwenye kulipa na adhabu, riba na faini kama ilivyo katika mazingira mengine.

MWISHO.